Ndoa, mimba za utotoni bado ‘mfupa mgumu’

Mtanzania - - Jamii Na Afya - Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

OKTOBA 11, kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, siku hiyo ilipitishwa rasmi mnamo mwaka 2012 na Baraza la Umoja wa Mataifa (UN).

UN ilianzisha siku hiyo maalumu kwa lengo la kuangazia shida na changamoto mbalimbali zinazomkabili mtoto wa kike ili kuzitatua na kuhamasisha jamii kuleta usawa kwa watoto wa jinsi zote (kike na kiume).

Jamii nyingi zinazoishi katika Bara la Afrika zinaamini kwamba mtoto ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu humjalia kila mwanadamu hapa duniani.

Lakini changamoto iliyopo ni kwamba si jamii zote ambazo zinawapa thamani sawa mtoto wa kike na wa kiume.

Kuna pengo kubwa katika suala la malezi huku mtoto wa kiume akionekana na kuchukuliwa (kulelewa) kama ndiye mwenye thamani kubwa zaidi kuliko mtoto wa kike katika familia nyingi.

Malezi ya mtoto wa kike hayapo sawa na yale ya mtoto wa kiume kwa mfano katika suala la elimu, wa kiume hupewa kipaumbele zaidi kuliko wa kike, jambo ambalo si sahihi.

Zipo jamii ambazo zinaona mtoto wa kike ni wa kusubiri kuolewa na kwenda kuishi na mumeme kujenga familia yake na hapa ndipo changamoto zaidi inapojitokeza.

Ni zipi?

Kutokana na pengo la malezi lililopo kati ya mtoto wa kike na wa kiume, tunashuhudia wengi wakikumbana na vitendo vya kikatili hasa ‘kulazimishwa’ kuolewa chini ya umri wa miaka 18.

Kwa mfano nchini Tanzania bado kuna mila na desturi ambazo zinaonekana wazi kumkandamiza mtoto wa kike kupata haki zake za msingi hasa elimu, afya bora na nyinginezo.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha asilimia 11 ya wanawake waliojifungua mwaka 2014 walikuwa na umri kati ya miaka 15 -19 duniani.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) ya mwaka 2016 inaweka wazi kwamba wasichana wana fursa ndogo ya kumaliza shule ikilinganishwa na wavulana.

Ripoti hiyo inaeleza wasichana wako katika hatari zaidi ya kukabiliwa na ndoa za utotoni, ajira za watoto, ukeketaji na matendo mengine ya udhalilishaji.

UNFPA inaonya kwamba vitendo hivyo vinadhoofisha na kuvunja haki za kibinadamu na afya ya msichana, wengi hushindwa kutimiza ndoto zao pindi wanapofikia umri wa kujitegemea hivyo kushindwa kuchangia katika shughuli za kimaendeleo kujenga uchumi wao binafsi, familia zao na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNFPA zaidi ya nusu ya wasichana milioni 60 walio na umri wa miaka 10 wanaishi katika nchi 48 zenye ukosefu mkubwa wa usawa wa kijinsia.

Hali ilivyo nchini

Licha ya serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoa elimu juu ya madhara yatokanayo na ndoa za utotoni hali inaonesha bado jitihada zaidi hasa kufikisha ujumbe kwa jamii zinahitaka.

Tafiti zinaonesha bado tatizo la ndoa za utotoni linazidi kuongezeka hali inayochangia pia ongezeko la mimba za utotoni ambazo zinatajwa pia kuchangia kwa namna moja au nyingi ongezeko la vifo vitokanavyo na uzazi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anasema takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Takwimu nchini hivi karibuni zinaonesha vifo hivyo vimeongezeka kutoka 432 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000.

Anasema hali hiyo inarudisha nyuma jitihada na malengo ambayo nchi ilijiwekea kupunguza vifo hivyo mpaka kufikia 193 ifikapo mwaka 2020.

“Ongezeko hili halikubaliki, hii inaashiria kunatokea vifo 900 kila mwezi sawa vifo 30 kila siku kutokana na uzazi, tumeanza jitihada kukabiliana na hali hiyo ikiwamo kuongeza vyumba vya upasuaji kufikia 170 ifikapo Juni 30, 2018,” anasema. Tanzania na maadhimisho Jana, Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambapo kitaifa yalifanyika huko Tarime mkoani Mara.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai anasema Mara ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo utafiti unaonesha kuna kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni.

Anasema utafiti wa Afya ya Uzazi na Utoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2015 unaonyesha, asilimia 27% ya watoto wa kike wanapata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18.

“Kulingana na utafiti huo, Katavi ndiyo mkoa ambao unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni kwa asilimia

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.