‘Awamu ya tano imeanza kurejesha mtizamo wa Nyerere’

Mtanzania - - Habari - Na THOBIAS ROBERT -MAELEZO

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, amesema Serikali ya awamu ya tano imeanza kurejea katika mtazamo wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya uchumi wa viwanda aliouanzisha.

Akizindua Kongamano la Kumbukizi ya Kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam juzi, Ole Nasha alisema Mwalimu Nyerere alijenga viwanda vingi hapa nchini.

Alivitaja viwanda ambavyo Mwalimu Nyerere alivijenga kuwa ni viwanda vya nguo kama Urafiki, Mbeya Tex, Mwatex, Mutex, viwanda vya ngozi, viwanda vya zana za kilimo, viwanda vya kutengeneza vipuli pamoja na viwanda vinavyotegemea malighafi za mazao yanayolimwa hapa nchini.

Alisema Taifa linahitaji viongozi wazalendo na waadilifu kama alivyo Rais Dk. John Magufuli ambaye ameonesha nia ya dhati ya kufuata nyendo za Mwalimu Nyerere kwa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi yanayotegemea viwanda.

“Serikali ya awamu ya tano kwa muda wa miaka miwili iliyokaa madarakani, imejitahidi kurejea na kuweka kwenye vitendo dhana ya Mwalimu Nyerere ya uchumi wa viwanda, kwani kwa sasa inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa, mwaka 2016/2017-2020/2021 unayojikita katika ujenzi wa viwanda kama njia ya maendeleo ya kiuchumi na maisha ya watu,”alisema Ole Nasha.

Alisema mtazamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni kutumia viwanda vya ndani kama njia ya kujinasua kutoka kwenye unyonyaji wa muda mrefu.

Kama Taifa huru kuna haja ya kuondoa tofauti za kisiasa na kuishi katika misingi ya usawa, umoja, ushirikiano ili kujiletea maendeleo ya uchumi kwa mtu mmoja na taifa kwa ujumla, ikiwemo kuhimiza uzalendo kwa kila mtanzania ili kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila, alisema kuwa ili kufikia Tanzania ya viwanda taifa linahitaji viongozi wazalendo wenye uchu wa maendeleo na wasio na misingi ya ukabila wala udini.

“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, hivyo ustawi wa uchumi wa viwanda unahitaji viongozi na watendaji ambao ni wazalendo, watiifu na wenye kutanguliza mbele masilahi ya taifa,”alisema Profesa Mwakalila.

Kongamano la maadhimisho ya siku ya Mwalimu Nyarere hufanyika kila mwaka ili kujadili busara, fikra na hekima zake katika kujenga usawa, maendeleo, umoja na ustawi wa uchumi wa taifa letu.

– PICHA: MPIGAPICHA WETU

MAONESHO: Mwanafunzi wa darasa la nne wa Shule ya Msingi Drive in ya Dar es Salaam, Mauren Rutta, akizungumza na wageni waliohudhuria maonyesho ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike yaliyoandaliwa na Taasisi ya HDIF, Dar es Salaam juzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.