Mvua yaleta maafa Kwimba

Mtanzania - - Habari / Tangazo - Na CLARA MATIMO -MWANZA

MVUA ya mawe iliyoambatana na upepo iliyonyesha katika Kijiji cha Manguluma, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, imejeruhi watu tisa na kuziacha kaya 135 bila makazi baada ya kuezua nyumba 179.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri, alisema jana, kwamba mvua hiyo ilinyesha usiku wa kuamkia Oktoba 10, mwaka huu na kuathiri pia majengo ya taasisi za Serikali.

Alisema mvua hiyo ilisababisha madhara kwa majengo mawili ya madarasa pamoja na maktaba katika Shule ya Msingi Manguluma, nyumba 29 katika Kijiji cha Lyoma na jengo la kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti.

“Mvua hiyo pia imeezua mapaa ya nyumba 24 za wakazi wa Mtaa wa Iramba, 13 za wakazi wa Mtaa wa Ngudulugulu pamoja na nyumba ya mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari, Igongwa iliyopo katika Kijiji cha Manguluma.

“Pia, imeezua choo cha shule hiyo, watu tisa wamejeruhiwa, kati yao, wanne wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya iliyopo mjini Ngudu.

“Kwa ujumla, baadhi ya wananchi wamepoteza mali zao, vyakula na wengine hawana sehemu za kuishi. Kwa hiyo, nawaomba watu walioguswa na tukio hilo, wawasaidie walioathirika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Pendo Malabeja, alisema wanaendelea kufanya tathmini ili kujua hasara iliyosababishwa na mvua hiyo na taarifa kamili wataitoa baada ya mhandisi wa ujenzi kufanya tathmini.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Shija Malando, alisema halmashauri yake itajitahidi kuwasaidia waathirika wa tukio hilo.

“Mimi wito wangu kama makamu mwenyekiti wa halmashauri, nawaomba wananchi wa wilaya hii, wapande miti ili kuzuia nyumba zao zisiendelee kuezuliwa na upepo kila wakati,” alisema Malando.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.