Uamuzi kesi ya Scorpion leo

Mtanzania - - Habari / Tangazo - Na FARAJA MASINDE - DAR ES SALAAM

UAMUZI mdogo katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi, ikiwamo kumtoboa macho Said Mrisho, inayomkabili Salum Njwete (34) maarufu ‘Scorpion’, unatarajiwa kutolewa leo baada ya wakili wa upande wa utetezi kushindwa kufika mahakamani jana.

Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Flora Haule kutokana na maombi yaliyowasilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga.

Aliomba uamuzi huo utolewe leo baada ya wakili Juma Nassoro wa upande wa utetezi kushindwa kufika mahakamani.

“Nimewasiliana na wakili Juma Nassoro wa upande wa utetezi na kuniahidi kuwa angekuwa amefika mahakamani saa 5.00, lakini amechelewa kutoka kwenye kesi Mahakama Kuu kutokana na uzito wa kesi hiyo.

“Hivyo akaomba kesi hii iendelee siku ya ijumaa (leo) ikizingatiwa kuwa mshtakiwa ana haki ya kuwakilishwa.

“Hivyo tunaomba kuwasilisha maombi hayo kama itakupendeza tuangalie kama tutaweza kufunga ushahidi wa kesi yetu hiyo kesho (leo),” alisema Katuga.

Hakimu Haule alikubaliana na maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi leo kama ilivyoombwa na upande wa utetezi.

Kesi hiyo ilifikia hatua hiyo baada ya upande wa utetezi kufungua kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi kutokana na kile ilichodaiwa ‘Scorpion’ alilazimishwa kutoa maelezo kwa nguvu katika Kituo cha Polisi Buguruni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.