AGENDA: Zebaki ni hatari kwa meno ya watoto

Mtanzania - - Habari / Tangazo - Na KHAMIS MKOTYA - DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Mazingira na Maendeleo (AGENDA), limeiomba Serikali kuzuia matumizi ya dawa ya kuziba meno yenye madini ya zebaki (mercury) kwa vile ni hatari kwa jamii hasa watoto.

Wito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Programu Mwandamizi wa shirika hilo, Dorah Swai, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Afrika ya kuhimiza tiba ya meno bila dawa yenye zebaki ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 13.

Dorah alisema Serikali ina wajibu wa kutekeleza Mkataba wa Kimataifa wa Minamata uliopitishwa na nchi 140 Tanzania ikiwamo, unaotaka kupunguza matumizi ya dawa yenye madini hayo inayojulikana kama ‘dental amalgam’.

Alisema lengo kuu la siku hiyo ni kuzitaka serikali za nchi za Afrika kusimamisha matumizi ya dawa ya kuziba meno hasa ya watoto na wanawake waliopo katika umri wa kuzaa.

Pamoja na mambo mengine asasi hizo ziliazimia kuwa Oktoba 13 kila mwaka iwe siku ya kukuza uelewa kuhusiana na kuondoa matumizi ya dental amalgam katika tiba ya meno.

“Zebaki (mercury) ni madini yenye sumu ambayo huathiri ukuaji wa ubongo wa watoto, mfumo wa hewa na mfumo wa fahamu hasa katika hatua ya ujauzito.

“Ni kwa sababu hii asasi hizi ziliweka siku hii kuzitaka nchi mbalimbali barani Afrika kuondoa matumizi ya dental amalgam katika kuziba meno na hasa ya watoto.

“Watoto wapo hatarini zaidi kuathirika na zebaki kwa kuwa ubongo wao bado unakua na pia wengi wao huathirika kupitia tumboni kwa mama, endapo mama ameingiwa na zebaki mwilini mwake.

“Zebaki huathiri ubongo na hata mfumo wa mishipa kwa binadamu wa rika zote, ila inaathiri zaidi watoto na moja ya matokeo yake ni kuwapunguzia watoto uwezo wa kufikiri,” alisema.

Aliongeza: “Hakuna sababu za kuendelea kutumia dawa hii kwa kuwa dawa nyingine ambazo hazina zebaki zipo barani Afrika na duniani kote.

Dawa hizo ni kama vile Composite Resin na Glassionomer. Kwa hiyo kuacha kutumia dawa hizi zenye sumu inawezekana”.

Ofisa huyo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kung’oa meno yanapokumbwa na hitilafu ya kutoboka kwa sababu mwanadamu anatakiwa kufariki dunia akiwa na meno 32 na si pungufu.

– PICHA: MPIGAPICHA WETU

MKATABA: Ofisa Programu Mwandamizi wa Shirika la AGENDA, Dorah Swai, akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) Mkataba wa Minamata unaozuia matumizi ya dawa zenye zebaki. Kushoto ni Ofisa Programu, Anneth Kweyamba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.