CCM Mara yaruhusu vitendo vya rushwa virekodiwe

Mtanzania - - Kanda - Na SHOMARI BINDA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara kimetoa ruksa kurekodiwa wagombea watakaofanya vitendo vya rushwa kuweza kupata ushahidi wa kuwaengua kuomba nafasi za uongozi.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Innocent Nanzaba amesema hatua hiyo imechukuliwa kukabiliana na wagombea watakaoanza kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo vya kutoa rushwa ili wachaguliwe,

Alisema wagombea wote walioomba nafasi za uongozi wamezuiwa kufanya kampeni kabla ya wakati na katika kukabiliana na hilo ni muhimu kubuni mbinu za kuhakikisha hilo linafuatwa.

Nanzaba alisema ili kupata ushahidi na kuchukua hatua kwa wagombea watakaokaidi wanachama wa chama hicho wafuatilie nyendo zao na kurekodi vitendo watakavyokuwa wanafanya, wao wenyewe au wapambe katika maeneo yao.

Alisema wapo wagombea ambao wanajiamini kuwa majina yao yatarudi kutoka ngazi ya taifa na kupitapita kwenye kata na wilayani ili kwenye uchaguzi wa mkoa waweze kuchaguliwa jambo ambalo maadili ya chama yanakataza .

Alisema kutokana na maendeleo ya mtandao wanachama wanaopingana na vitendo visivyofaa ndani ya chama wanapaswa kuwasaidia viongozi kwa kuwabaini wagombea hao kwa kuwarekodi kupata ushahidi wa kubaini makosa yao na kuenguliwa kwenye uchaguzi.

“Tunaomba wanachama wetu watusaidie kuweza kuwakamata wagombea ambao wanashindwa kufuata maadili na maelezo ya chama na ili kuwapata mtakapowaona muwarekodi tupate ushahidi na kupeleka panapohusika.

“Makatibu wa CCM kule kwenye ngazi ya wilaya pia wanapaswa kutusaidia kupata taarifa za wagombea hao kwa kuwa huko kwenye wilaya ndiko kunaweza kutokea vitendo vya kuanza kampeni mapema na kutolewa rushwa,”alisema Nanzaba. Alisema wanachama 24 wamejitokeza kuomba nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara,19 wanawania nafasi ya halmashauri kuu ya taifa (NEC) na 16 wanawania nafasi ya katibu wa itikadi na uenezi.

– PICHA: SHOMARI BINDA

ELIMU: KATIBU wa CCM Mkoa wa Mara, Innocent Nanzaba, akizungumzia hatua ya kurekodiwa kwa wagombea wa chama hicho watakaoanza kampeni kabla ya muda au kujihusisha na vitendo vya rushwa, ili kupata ushahidi wa kuwaengua.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.