Wazee walalamikia mgogoro wa viongozi Wilaya ya Gairo

Mtanzania - - Mkoa - Na RAMADHAN LIBENANGA

BARAZA la wazee washauri wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro, wameiomba Serikali kuchukua hatua za kumaliza mgogoro wa kiutendaji uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Siriel Nchembe na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo.

Wakizungumza na MTANZANIA juzi, mmoja wa wazee hao, Yakob Masele, alisema kama hatua za haraka hazitachukuliwa, mgogoro huo unaweza kudhoofisha maendeleo wilayani hapa.

“Baadhi ya viongozi mkoa na Taifa, wamekuwa wakilikemea tatizo hilo, lakini tunaona bado halijatatuliwa.

“Kwa hiyo, tunazidi kuwaomba viongozi wetu wa ngazi za juu, waendelee kuufanyia kazi huu mvutano kwa sababu unarudisha nyuma maendeleo ya wilaya yetu. “Nayasema haya kwa sababu Gairo ina changamoto nyingi, ikiwamo ya upatikanaji wa maji na miradi mingi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, lakini imekuwa ikisuasua kwa sababu ya kutokuwapo kwa ushirikiano kati ya mkuu wa wilaya na baadhi ya watendaji.

“Mkuu wetu wa wilaya anapokuta changamoto mahali, hawezi kuwatafuta viongozi wenzake ili waangalie namna ya kuzitatua, badala yake anaagiza wakamatwe na kuwekwa ndani bila kufunguliwa mashtaka yoyote,” alisema Masele.

Naye mzee Silvan Chitemo (60), alisema mgogoro huo wa uongozi umesababisha wananchi washindwe kufanya kazi na Serikali yao kwa hofu ya kuwekwa ndani kwa amri ya Mkuu wa Wilaya yao.

“Mkuu wa Wilaya amekuwa akifanya kazi kwa vitisho zaidi kwa kutumia polisi na kuwafanya baadhi ya viongozi, wakiwamo wa vitongoji, vijiji na kata, kukataa majukumu yao kwa hofu ya kukamatwa na polisi,” alisema mzee Chitemo.

Alipotakiwa kuzungumzia malalamiko hayo, Mkuu huyo wa Wilaya, Nchembe, alisema aliagiza Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magoweko na msaidizi wake wawekwe ndani ili kuokoa maisha yao kwa kuwa wananchi walitaka kuwapiga.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Agnes Mkandya, alipohojiwa kuhusu malalamiko hayo, hakuwa tayari kuyazungumzia, kwa madai kuwa kamati ilishaundwa ili kuyafuatilia.

PICHA: MPIGAPICHA WETU

RAMANI: Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula akikagua vifaa vya uchapaji na uandaaji wa ramani vya Chuo cha Ardhi Tabora vilivyogharimu kiasi cha Sh milioni 200.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.