Madaba kupata umeme kabla ya Krismasi

Mtanzania - - Mkoa - Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema litawasha umeme katika Halmashauri ya Mji wa Madaba, wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, kabla ya sikukuu ya Krismasi mwaka huu.

Hayo yameelezwa jana mjini hapa na Meneja Mradi wa Umeme wa MakambakoSongea wa KV 220, Didas Lyamuya, alipokuwa akizungumza mjini hapa.

Alisema kwamba, lengo la mradi huo ni kupeleka na kuboresha umeme katika maeneo ya uzalishaji na majumbani kwenye vijiji vilivyopo katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Alisema kwamba, kukamilika kwa mradi huo kutakuwa ni ukumbozi kwa wananchi na wawekezaji wa sekta ya viwanda ambao watapata umeme wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji.

“Madaba kwa sasa ni halmashauri na Serikali iliagiza tuunganishe umeme na sasa kama mnavyoona, tayari tumeshasambaza miundombinu yote na kazi

iliyobaki ni kuunganisha majumbani.

“Mradi wa eneo hili hautosubiri mradi wa Makambako-Songea, ila tutawaunganishia Novemba au Desemba mwaka huu.

“Lengo letu ni kwamba, tunahitaji hapa Madaba waweze kusherehekea sikukuu ya Krismasi wakiwa na umeme majumbani.

“Tulifanya uhakiki mwaka 2014 na kubaini hapa Madaba mjini pekee kuna nyumba zaidi ya 700 na sasa zimeongezeka na kufika zaidi ya 1,000 na zote tutaziunganisha kwa umeme, kwani sasa tunafunga jenereta,” alisema Lyamuya.

Pamoja na hayo, alisema bado wanaendelea kuunganisha umeme kwa wawekezaji wa viwanda kwa lengo la kuimarisha uzalishaji, kwa kuwa na umeme wa uhakika.

Kutokana na hali hiyo, Lyamuya alisema tayari wamefanikiwa kufunga umeme katika Kiwanda cha Chai Kabambe, baada ya kutolewa agizo na Waziri wa Nishati, Dk. Merdad Kalemani na kufanikiwa kuunganisha umeme huo kwa muda wa wiki mbili.

Akizungumzia mradi wa umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Madaba, Lyamuya alisema mradi huo utakapokamilika, utanufaisha vijiji zaidi ya vinane, ingawa kwa sasa wamekuwa na mazungumza na watendaji wa Idara ya Misitu, kwani sehemu ya mradi huo itapita kwenye Msitu wa Wino.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.