Umuhimu wa kujiimarisha katika mbinu za utambuzi

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - Na KIZITO MPANGALA

KESI ya Almasi ni riwaya iliyoandikwa na Profesa Rao Shaoping kutoka China yenye jumla ya kurasa 184. Kimegawanywa katika sura 10 katika mtiririko wa matukio. Kimepewa namba za usajili ISBN 978-9976-60-579-2 na kuchapishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUP).

Kitabu hiki kinaelezea kuhusu kesi ya mauaji ya kijana Rashidi, ambaye aliuawa kwa kuwa alikuwa akimiliki vipande 10 vya madini ya almasi aliyoachiwa na baba yake mzazi kama urithi.

Lakini madini hayo yaliyosababisha kifo cha Rashidi yamekuwa na historia ya miaka kadhaa nyuma, kwa maana hiyo basi yalikuwa yakitunzwa kimagendo mpaka yalipokuja kuwa mikononi mwa polisi.

Profesa Rao Shaoping ameonyesha umahiri na umuhimu wa taaluma ya upelelezi na kuiweka katika mazingira ya kuwa si kazi ya kuisitisha unapopata ushahidi kwa haraka.

Ni kazi inayohitaji ufundi na uigizaji ili kumpata mhalifu. Profesa Shaoping anatoa rai kwa askari polisi kwamba kazi ya upelelezi inahitaji ubunifu wa kijanja zaidi na kujiamini, pia itamlazimu mpelelezi asome maandiko mbalimbali ili kujiimarisha katika mbinu za utambuzi.

“Inspekta hodari lazima awe na ujuzi mbalimbali, hata ujuzi wa lugha, lazima asome vitabu mbalimbali pengine hata kamusi,” (Uk. 71 – 72)

Mwandishi anaweka wazi kwamba upo uwezekano mkubwa wa maafisa wa polisi wastaafu au wale walioachishwa kazi kwa makosa mbalimbali kuweza kujihusisha na biashara za magendo na hivyo kuwa na weledi katika mambo ya upelelezi jambo ambalo husababisha kutogundulika haraka.

Anasema wanaweza kukaribisha wageni wa kutoka nchi za nje ambao wanahusiana nao katika shughuli za biashara za magendo.

Mwandishi anasema hifadhi ya wanyama ya Saanane huko Mwanza iangaliwe kwa macho ya pekee katika ulinzi.

Mwandishi anatoa rai na morali kwa askari wetu kujituma katika kazi ya ulinzi na upelelezi. Sasa hivi tupo katika ulimwengu uliorahisishwa katika mawasiliano, hivyo ni rahisi sana kwa wahalifu mbalimbali kuwasiliana na wahalifu wenzao nchi za nje na wakija huwa wanabadilisha majina ili wasitambulike.

Hivyo basi, majeshi yetu ni vema yakawa macho katika usalama wa taifa letu, na wananchi hawapaswi kukaribisha tu wageni wa nchi za nje bila utaratibu maalumu utakaolinda usalama.

Kazi ya upelelezi inaweza kuchukua muda mrefu, hii ni kutokana na ukweli kwamba ushahidi mwingine unaweza kupatikana mbali na eneo la tukio. Hivyo basi askari wetu na maafisa wa usalama hasa Afrika wamakinike.

“Wakati mwingine upelelezi wa kesi fulani haujikiti tu kwenye eneo la tukio, ikiwa ni lazima, inabidi kupanua wigo wa upelelezi,” (Uk.19).

Inspekta Kazinjema alimakinika na ukweli huu na akafanikisha mchakato wote bila kujali rangi, cheo, umri wala jinsia ya mtu. Hivyo basi maafisa wa usalama wamakinike na ukweli huu kwa kuiga mfano wa Inspekta Kazinjema katika kitabu hiki.

Askari wanaofanya kazi ya upelelezi nao ni binadamu wanahitaji muda wa kupumzika, pia wanayo mambo mengine yanayowahusu wanahitaji kuyakamilisha katika maisha yao.

Mwandishi amesisitiza uvumilivu hasa kwa upande wa akina dada. Unapoona jambo muhimu mpenzi wako anaahirisha usiwe mstari wa mbele kulalamika. Mwandishi anataka ufuate mfano wa binti Rabeka katika uvumilivu na hatimaye akakamilisha methali ya isemayo ‘mvumilivu hula mbivu’.

Riwaya hii yawezekana ikafananishwa na filamu maarufu iliyoigizwa sehemu mbalimbali ikiwemo Sierra Leone, Gabon, na Uingereza ikielezea mapigano yanayojitokeza migodini, filamu hiyo inaitwa ‘The Blood Diamond’.

Kwa hiyo, huenda almasi ni madini ambayo yanaweza kuhamisha mito, mabonde na milima na kuiangushia upande mwingine.

Almasi inaweza kuondoa uhai wa wengine. Huko migodini wachimbaji wapendane na washirikiane kikamilifu katika kazi kama vile Inspekta Kazinjema alivyoshirikiana kikamilifu na askari wenzake, bwana Kawa na Yasini.

Mwandishi anatoa msisitizo wa kuzungumza lugha ya Kiswahili ili mawasiliano yawe kwa ukamilifu. Hivyo basi, hata katika kazi za upelelezi Kiswahili kitumike ili kupata taarifa zaidi na vilevile si vibaya kutumia lugha nyingine itakapobidi. Maafisa wa usalama wamakinike na ukweli huu ili nao waweze kuwapa morali wasaidizi wao kwa ushirikiano mzuri.

Wapo wanawake wanaoishi maisha ya anasa bila kujishughulisha. Katika wanawake wa aina hiyo wapo wanaotumika katika kazi za magendo ili kukamilisha uhalifu wa aina mbalimbali. Wanatumika kwa njia mbalimbali ikiwemo kufanya mapenzi na wanaume kadhaa wanaohusika katika biashara za magendo kisha hufurahia fedha wanazopewa huku maisha yakiendelea.

Mara nyingi wanawake hao huwa na mwisho mbaya. Hivyo basi, wanawake wamakinike na shughuli halali za kupata ridhiki zao. Kujihusisha na biashara za magendo si jambo nzuri.

Kuleweshwa na sifa za utendaji kazi kunaweza kukusababishia kufanya vibaya na kuweza kupoteza fursa ya kupata fununu mbalimbali. Kwa hiyo, kwa sifa yoyote utakayopewa popote basi usimakinike na ulevi wake. Sisi sote tumakinike na ukweli huu.

Kwa kuhitimisha, mwandishi ametoa funzo kubwa la jinsi ya kukabiliana na upelelezi wa kesi mbalimbali hasa zinazohusu mauaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.