BoT yawapiga msasa walemavu

Mtanzania - - Kanda - Na GURIAN ADOLF

WATU wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) mkoani Rukwa, wameishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwapa mafunzo maalumu ambayo yamewajengea uwezo wa kutambua namna bora ya kuhifadhi fedha.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika jana, yalihusisha watu wenye ulemavu wa kutosikia, ambapo walifundishwa namna bora ya kuhifadhi fedha pindi waendapo katika matumizi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja Msaidizi wa Idara ya Fedha wa BoT, Vick Msina, alisema watu wengi wamekuwa hawajui namna bora ya kuweka fedha, wamekuwa wakizikunja na kuziweka mifukoni ama wanawake kuzifunga katika kanga walizovaa, kitendo kinachosababisha fedha hizo kuchakaa mapema.

Alisema ni vizuri mtu yeyote anapokuwa anakwenda kufanya manunuzi akawa anabeba fedha kwenye pochi zikiwa zimenyooka, badala ya kuzikunja na kuweka mfukoni, kuweka miguuni kwenye soksi au kwenye sidiria, kwani kufanya hivyo kunasababisha fedha kuchakaa haraka.

Alisema suala hilo si tu kwa watu wenye ulemavu wa kusikia, bali ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa anazitunza fedha vizuri ili zitumike kwa muda mrefu.

Naye Mwenyekiti wa Viziwi Mkoa wa Rukwa, Henry Kisusi, alisema mafunzo hayo yamekuwa nimuhimu sana kwao, kwani wamekuwa hawapati fursa nyingi na hivyo kujikuta wakitumia vibaya fedha hizo pamoja na kubambikiziwa fedha bandia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.