TCDC kutokomeza mimba za utotoni Katavi

Mtanzania - - Kanda - Na WALTER MGULUCHUMA

SHIRIKA Lisilo la Kiserikali la TCDC limezindua mkakati wa kutokomeza mimba za utotoni mkoani Katavi, kwa kuwa mkoa huo unaongoza kwa idadi kubwa ya mimba za utotoni.

Mkakati huo ulizinduliwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ambayo kimkoa yalifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashaulili, Manispaa ya Mpanda.

Mwakilishi wa TCDC, Nazar Yusuph, alisema wameamua kuzindua mkakati huo mkoani Katavi, kwa kuwa bila kufanya hivyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi. “Takwimu zinaonyesha Mkoa wa Katavi unaongoza kitaifa kwa mimba za utotoni ukilinganisha na hali hiyo katika mikoa mingine nchini.

“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana shirika letu limeamua kuweka mpango wa kumaliza tatizo la mimba za utotoni na tutafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa pamoja na halmashauri zote mkoani hapa,” alisema Nazir. Nazir alizitaja baadhi ya sababu zinazochangia Mkoa wa Katavi kuwa na mimba nyingi za utotoni, kuwa ni shule nyingi za sekondari kutokuwa na mabweni ya wanafunzi wa kike na wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu kufuata shule.

“Sababu nyingine ni tamaduni za baadhi ya makabila yaliyoko mkoani hapa ambayo huwaoza watoto wao kwa ajili ya kujipatia kipato bila kujali umri walionao watoto wao,” alisema Nazir.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.