Utafiti wa WB waonyesha DART inahudumia watu 400,000 kwa siku

Mtanzania - - Biashara - NA AZIZA MASOUD

UTAFITI uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) umeonyesha kuwa, mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART) awamu ya kwanza uliopo jijini Dar es Salaam umepata mafanikio makubwa na sasa una uwezo wa kuhudumia watu 400,000 kutoka 200,000 kwa siku.

Akizungumza jana, mtaalamu aliyeongoza timu ya wataalamu waliofanya utafiti huo, uliokuwa ukiangalia tathmini ya utendaji kazi wa DART, James Rayner, alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo, mradi huo una uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu, tofauti na ilivyoelezwa awali.

“Endapo uendeshwaji wa mradi wa DART ukifanyika kikamilifu, zaidi ya wananchi 400,000 watakuwa na uwezo wa kutumia usafiri huo kwa siku,” alisema Rayner.

Alisema mbali na kuongezeka kwa idadi ya watu, utafiti huo pia ulibaini uwepo wa wateja wengi katika kituo cha Kimara, ambapo watu wanaopanda eneo hilo wamefikia 28,000 kwa siku.

Alisema utafiti huo pia ulionyesha asilimia 33 ya abiria wote wanapanda katika vituo vikuu vinne vya Kimara, Msimbazi Polisi, Gerezani na Kivukoni.

Kwa upande wa Mratibu wa Mradi wa Uendelezwaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Emmanuel Ndyamukama, alisema utekelezaji wa mradi wa DART, unakwenda sambamba na uboreshwaji wa jiji hilo katika maeneo mbalimbali, hasa yenye msongamano wa watu.

Alisema maeneo ambayo yatafaidika na maboresho ya mradi wa DART ni pamoja na Tandale, Manzese, Mwananyamala, Ukonga, Mburahati na Mbagala.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.