Wateja waisababishia Tanesco hasara ya milioni 116/-

Mtanzania - - Habari -

SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) katika Mkoa wa Dar es Salaam, limekamata wateja 116 waliokuwa wakitumia umeme bila kulipia na kulisababishia shirika hilo hasara zaidi ya Sh milioni 116.

Wateja hao wamekamatwa katika operesheni inayoendeshwa na shirika hilo ya kukagua mita za umeme kwa wakazi wa jiji hilo.

Akizungumza katika operesheni hiyo, Mkaguzi na Udhibiti wa Mapato Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Mrisho Sangiwa, alisema operesheni hiyo imeanza Septemba 26 mwaka huu, huku ikiwafikia wananchi 5,444.

Alisema lengo la operesheni hiyo ni kuangalia miundombinu ya shirika hilo kwa Kanda ya Mkoa huo kwa kila mtumiaji wa umeme.

“Kati ya watumiaji 5,444 wa umeme, mita 49 zimekutwa hazitumii umeme vizuri.

“Tumebadilisha mita zaidi ya 100 huku tukiangalia hesabu iliyopatikana kwa wateja waliokuwa wana matatizo ni zaidi ya Sh milioni 166 hadi leo (jana) na robo ya fedha hizo zimeshalipwa,” alisema Sangiwa.

Alisema operesheni hiyo itafika kwa kila mtumiaji wa umeme katika mikoa hiyo miwili, ambapo mteja atakayekutwa akiiba umeme atachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya umeme ya mwaka 2008, ni kosa kisheria kuingilia miundombinu ya shirika. Mhandisi Sangiwa alisema wananchi wanapaswa kuepuka vishawishi vya vishoka kwa kuwaunganishia umeme bure kwani kunaweza kusababisha milipuko na kuunguza nyumba.

Alisema miundombinu ya umeme ni gharama kwa wananchi hivyo wanapaswa kuipenda ili kulipa kodi serikalini kwa kulipa bili na hata kusaidia wananchi wasiokuwa na umeme kuunganishiwa nishati hiyo hadi vijijini.

“Wananchi tuungane kupiga vita wizi wa umeme na huu mchakato ni endelevu, msishawishiwe na vishoka kwa kuwawekea umeme bure, vishoka ni mafundi ambao wengi wao hawajasajiliwa, wananchi wawe makini,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.