Argentina wamsamehe Lionel Messi

Mtanzania - - Habari -

MASHABIKI na wadau wa soka nchini Argentina, wametumia mitandao ya kijamii na kudai wamemsamehe mshambuliaji wao, Lionel Messi, kwa kushindwa kuimba wimbo wa Taifa katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Ecuador.

Mchezo huo uliopigwa Jumanne wiki hii, Argentina walifanikiwa kufuzu baada ya mchezaji huyo kupachika mabao matatu peke yake, lakini kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa video ambayo inamwonesha Messi akishindwa kuimba wimbo wao wa Taifa kabla ya kuanza kwa mchezo huo.

Messi alionekana akiwa anainamia chini huku wenzake wanaimba wimbo huo kitendo kilichopelekea kujadiliwa na wachambuzi mbalimbali wa soka nchini humo, huku wengine wakisema kuwa ni utovu wa nidhamu na kukosa heshima.

Lakini kutokana na mchezaji huyo kuonesha kiwango cha hali ya juu na kuipeleka katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani kutokana na mabao yake, mashabiki wameweka wazi kuwa hawana tatizo na mchezaji huyo na wamemsamehe kutokana na aibu aliyowaondolea.

Tangu Argentina ifanikiwe kufuzu kwenye mchezo huo, mashabiki mitaani wanaonekana wakiwa wamevaa jezi ya mchezaji huyo yenye namba 10 mgongoni.

Hata hivyo, Shirikisho la soka nchini humo, limejaribu kumkingia kifua kwa kusema kuwa maisha ya mchezaji huyo yamekuwa nchini Hispania kwa muda mrefu, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kukosea wakati wa kuimba wimbo huo na wenzake.

Mchezaji huyo aliondoka nchini Argentina akiwa na umri wa miaka 13 na kujiunga na kikosi cha Barcelona nchini Hispania na

sasa ana umri wa miaka 30, hivyo kwa kipindi hicho chote ambacho amekuwa nchini Hispania wanaamini ana uwezekano wa kusahau baadhi ya maneno kwenye wimbo wa Taifa.

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa endapo mchezaji huyo angeshindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu basi angechukuliwa hatua kwa kushindwa kuimba wimbo huo au angeshambuliwa na idadi kubwa ya mashabiki.

Jumatano wiki hii Argentina waliendelea kusherehekea kufuzu Kombe la Dunia, hivyo baadhi ya magazeti nchini humo yalikuwa na vichwa vya habari mbalimbali kama vile ‘Asante Messi’, ‘Argentina ni ya kwako Messi’, ‘Messi ni Genius’ na mengine mengi.

Hadi sasa mchezaji huyo amefunga ‘hat trick’ tano katika timu ya Taifa, mara ya kwanza alipachika mabao matatu kwenye mchezo dhidi ya Switzerland, Februari 2012, Brazil (Juni 2012), Guatemala (Juni 2013) na Panama (Juni 2016) huku ya tano ikiwa dhidi ya Ecuador Oktoba 10 mwaka huu.

Messi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.