‘Maalim Seif hapimwi akili, mkojo’

Mtanzania - - Mbele - Na MWAJUMA KOMBO - ZANZIBAR

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad hana tatizo la ugonjwa wa akili na kwa kudra za mwenyezi Mungu ataiongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa chama hicho Wilaya ya Mjini Unguja.

Katika hotuba yake ya kufungua mkutano huo, Mazrui alisema afya ya Maalim Seif ni madhubuti, akili yake ipo safi na hana mpango wa kupimwa akili wala mkojo.

Kauli hiyo ya Mazrui inajibu taarifa zinazosambazwa na wanaoaminika kuwa mahasimu wa kisiasa wa Maalim Seif na CUF zikieleza kuwa Katibu Mkuu huyo ana ugonjwa wa akili ndiyo maana amekuwa akitoa kauli za kuuota urais wa Zanzibar.

Taarifa ambazo zimekuwa zikisambaa hasa kwenye mitandao ya kijamii baada ya Maalim Seif kueleza kuwa anatarajia kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar hivi karibuni zinaeleza kuwa kiongozi huyo huenda anasumbuliwa na maradhi ya akili hivyo anapaswa kupatiwa tiba.

Lakini Mazrui katika majibu yake ya jana kuhusu madai hayo alisema yeye ndiye anayekaa na Maalim Seif hivyo anajua haumwi na kwamba wanaendelea na maandalizi ya kuongoza serikali.

“Mimi ndiye ninayekaa na Maalim Seif, yupo madhubuti na akili yake ni nzuri. Hapimwi akili wala mkojo, sisi kama wanachama tunamuamini, tuna uhakika kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu ataiongoza.

“Kama kuna mtu anaona Maalim anasema uongo juu ya kauli zake, asimame mbele za watu na kuthibitisha hilo kama kweli Katibu Mkuu anasema uongo,” alisema Mazrui.

Akizungumzia chockochoko za wapinzani wao wa kisiasa, alisema wanapitapita wakiwajaza maneno ya chokochoko wanachama wao kuwa Maalim ni muongo ili wawavunje moyo.

Alisema hawayumbishwi wala hawaogopi na Maalim Seif hajavunjika moyo wala hajatetereka kwa kauli hizo.

“Sisi hatushawishiki na aliyekuwa hodari aje asimame mbele kama nilivyo simama mimi, aje aseme kama Maalim Seif anasema uongo.

“Msiyumbishwe na maneno ya watu hao na waendelee kumshika mkono Maalim Seif kwa kuwa kazi aliyonayo ni ngumu.

“Maaalim Seif yupo imara na anasimamia haki yetu, msiyumbishwe kwani mwenye kusubiri hajuti, wanaokaa na kujidanganya sisi tushajiandaa kuchukua serikali na kama watendaji wakuu tumejipanga kumsaidia kuiendesha serikali hiyo,” alisema Mazrui.

Alisisitiza kuwa hatua waliyofikia kama chama hawawezi kurudi nyuma na kwamba atakaye rudi nyuma chujio litamchuja.

“Hatupambani kwa vita bali tutatumia njia sahihi za kupata haki yetu,” alisisitiza.

Kuhusu uwezo wa chama kujiendesha alisema ingawa CUF hakipati ruzuku kutoka serikalini bado kiko imara na kutoa mfano wa mikutano mikuu ya matawi na wilaya inayoendelea kufanyika kwa gharama za chama bila kupokea ruzuku.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.