MICHEZO

Mtanzania - - Habari -

Joshua amchapa Takam kwa TKO

HATIMAYE bingwa wa ngumi uzito wa juu nchini Uingereza, Anthony Joshua, amefanikiwa kutetea taji lake la IBF baada ya kumchapa mpinzani wake, Carlos Takam raia wa nchini Cameroon.

Joshua aliweza kushinda katika raundi ya 10 kwa TKO, kama alivyotarajia awali kabla ya kuanza kwa pambano hilo.

Pambano hilo lilifanyika ikiwa ni siku 12 baada ya kusitishwa kwa pambano kati ya Joshua na Kubrat Pulev kwa sababu ya Pulev kusumbuliwa na tatizo la bega, hivyo Takam akaamua kujitokeza na kuchukua nafasi ya Pulev.

Hata hivyo, baada ya Pulev kujitokeza, Joshua aliweka wazi kuwa lazima ashinde na hataweza kumaliza raundi ya 10 kabla ya kumaliza pambano hilo.

Pambano hilo la mwishoni mwa wiki lilionekana kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na wawili hao kutupiana makonde ya nguvu, huku Takam akionekana kuvuja damu mdomoni na Joshua kuvuja damu puani.

“Kazi yangu kubwa ilikuwa kuhakikisha ninashinda pambano hilo bila ya kujali raundi ya ngapi, mpinzani wangu alikuwa na ushindani wa hali ya juu lakini niliweka wazi mapema kwamba nitamaliza pambano hilo kabla ya kumalizika kwa raundi ya 10,” alisema Joshua.

Katika ushindi huo, Joshua alifanikiwa kuondoka huku akiwa na pointi 87, wakati huo mpinzani wake Takam akifanikiwa kujipatia pointi 83.

Joshua na Promota wake Eddie Hearn, wamedai kuwa wapo kwenye mipango ya kutangaza mpinzani wa pambano lijalo mwakani kati ya bingwa wa mkanda wa WBC, Deontay Wilder au Tyson Fury.

“Nadhani tayari nimewapa mashabiki wangu kile ambacho walikuwa wanakitaka, hivi karibuni tutamweka wazi mpinzani wetu kwa ajili pambano la mwakani. Baada ya ushindi huu kinachofuata ni maandalizi ya pambano lingine, promota wangu yupo tayari kutafuta mpinzani,” aliongeza.

Kwa upande wa Takam baada ya kukubali kichapo hicho, alimpongeza mpinzani wake huku akidai amejifunza mengi kutoka kwake baada ya mchezo huo.

“Nilikuwa na uhakika wa kushinda, lakini ninaamini mpinzani wangu alikuwa bora zaidi yangu, hivyo Joshua alistahili kuwa bingwa na nitakuwa nimejifunza mengi kutoka kwake,” alisema Takam.

Pambano hilo la juzi lilikuwa la 20 kwa Joshua katika maisha yake ya ngumi za kulipwa, hivyo ameweka historia ya kushinda jumla ya mapambano yote kwa KO na hajawahi kupoteza hata moja.

Joshua

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.