Wabunge wahoji msafara wa rais

Mtanzania - - Habari - Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

BAADHI ya wabunge, wamehoji utaratibu unaotumika kuyapa nafasi ya mbele magari ya wakuu wa mikoa na wilaya huku yao yakiwekwa nyuma wakati msafara wa rais unapokuwa katika majimbo yao.

Hoja hizo ziliibuliwa jana na wabunge hao wakati wakichangia kwenye semina ya wabunge ya diplomasia na itifaki iliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Semina hiyo iliwashirikisha wawakilishi kutoka vyama vya kibunge, wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Wa kwanza kuibua hoja hiyo alikuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM) ambaye alihoji namna magari yanavyopangwa kwenye msafara wa rais.

“Gari la mkuu wa mkoa huwa linakuwa mbele likiwa na bendera na hufuatiwa na gari la mkuu wa wilaya na magari ya wabunge huwa ni ya mwisho.

“Katika hili tunaomba ufafanuzi ni kwanini gari la mbunge huwa la mwisho katika ziara,” alihoji Aeshi.

Nao wabunge Ester Matiko wa Tarime Mjini, (Chadema) na Cecilia Pareso wa Viti Maalum, waliunga mkono hoja hiyo na kutaka ufafanuzi kama alivyoomba Aesh.

Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah (CUF), aliomba apewe ufafanuzi kuhusu itifaki.

Wakati wabunge hao wakiuliza hayo, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (CCM), alisema wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wana mamlaka ya kupeperusha bendera katika msafara wa rais kwa sababu ni wateule wa rais.

“Rais anachaguliwa na watu wa nchi nzima tofauti na mbunge ambaye anachaguliwa na watu wa jimbo lake tu.

“Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, wanamwakilisha rais aliyechaguliwa nchi nzima, wakati sisi ni wawakilishi wa vijimbo tu.

“Lakini pia, viongozi hao ndiyo viongozi pekee wenye kofia mbili kwa maana ya ukuu wa serikali wa eneo husika na pili ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao,” alisema Mgumba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.