Azikwa mkono ukichomoza juu ya kaburi Mbeya

Mtanzania - - Habari - Na PENDO FUNDISHA -MBEYA

MWILI wa mwanamume asiyejulikana, umekutwa umefukiwa ndani ya shimo linalofanana na kaburi, kisha mkono wake mmoja ukichomoza juu ya kaburi.

Tukio hilo la aina yake, limetokea juzi saa moja usiku katika Kata ya Ghana, Tarafa ya Sisimba mkoani Mbeya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo chake.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hili, maana haiwezekani mtu kazikwa na watu wasiojulikana, kisha kuacha mkono ukionekana juu ya kaburi,” alisema Kamanda Mpinga.

Wakizungumza na gazeti hili, mashuhuda wa tukio hilo walisema wao walisikia kelele za kuomba msaada zilizokuwa zinatolewa na jirani mwenzao, jambo ambalo liliwapa mshtuko mkubwa.

Walisema walipofika kwenye nyumba hiyo, walielezwa kwamba kuna mwili umefukiwa ndani ya shamba lililokuwa nje ya nyumba ya mwanamama huyo na walienda kushuhudia na kufanikiwa kuukuta mkono huo ukiwa juu ya eneo lililotengenezwa kama kaburi na kisha kutoa taarifa polisi.

“Nikiwa ndani naendelea na shughuli zangu, nilisikia kelele za watoto wakikimbia na wengine waliingia ndani na kunieleza kwamba wameona mkono wa mtu upo nje ya shamba dogo lililo nje ya nyumba, nilitoka kwenda kuangalia na kweli niliukuta mkono huo na ndipo nilipopiga kelele za kuomba msaada kwa wananchi,” alisema.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama huyo, anasema watoto hao walikuwa wakicheza nje ndipo walipouona mkono huo ukiwa unaonekana umefukiwa na udongo, lakini bado ulikuwa nje na juu ya kaburi hilo.

Aidha, imeelezwa kwamba askari polisi walifika kwenye eneo la tukio, kisha kuufukua mwili huo na kuupeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha mwili wa mwanamume huyo kwa nje ulikuwa na majeraha ya kupigwa na vitu vyenye ncha kali.

Hata hivyo, akizungumzia mauaji hayo, Diwani wa Kata ya Ghana, Fabiani Sanga, aliwataka wakazi wa eneo hilo na wananchi wa Mkoa wa Mbeya kufika hospitali kwa ajili ya kuutambua mwili wa marehemu huyo.

– PICHA: FLORENCE SANAWA

MNADA: Wakulima wa Korosho wa Kijiji cha Dihimba Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, wakifungua sanduku lenye barua za wanunuzi wa korosho katika mnada wa pili mkoani Mtwara juzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.