Sugar waonja ushindi wa kwanza VPL

Mtanzania - - Mbele - Na MOHAMED KASSARA

KAGERA Sugar wameonja ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), baada ya kuifunga mabao 2-1 Ndanda katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.

Katika mchezo huo, mabao ya Kagera Sugar yalifungwa na Venance Ludovick na Edward Christopher, huku bao la Ndanda likifungwa na Omary Mponda kabla ya Ludovick kuisawazishia Kagera Sugar dakika ya 50 na Christopher kuongeza bao la ushindi dakika ya 80. Kwa matokeo hayo Kagera Sugar wamefikisha pointi sita na kupanda hadi nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hiyo.

Kagera Sugar ilipata ushindi huo baada ya kuanza vibaya ligi hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na Mbao FC, kabla ya kupata sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting.

Baadaye walifungwa bao 1-0 na Azam na kufungwa bao 1-0 na Singida United, kabla ya kupata sare tasa na Majimaji na kufungwa mabao 2-1 na Yanga na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Mwadui. Katika mchezo mwingine, Lipuli iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora, mkoani Iringa.

Mbao FC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 10 kupitia Habibu Kondo, kabla ya beki wa Lipuli, Asante Kwasi, kusawazisha kwa penalti dakika ya 73 baada ya Seif Karie kuangushwa eneo la hatari.

Baadaye mchezaji wa Mbao FC, Ndaki Robert, alijikuta anajifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira kwa kichwa.

Kutoka Uwanja wa Majimaji mjini Songea, wenyeji Majimaji walitoka sare ya kufunga bao 1-1 na Mwadui FC huku Mtibwa Sugar wakitoka sare tasa na Singida United kwenye Uwanja wa Manungu na Njombe Mji walipata matokea kama hayo dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Sabasaba, mjini Njombe.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.