Kipofu wa miaka 10 amkana mkewe

Adai ni mzee, afanya ziara kukagua mitaa

Mtanzania - - Mbele - Na WALTER MGULUCHUMA -KATAVI

Nkondwa Sikazwa (78), Mkazi wa Mtaa wa Kawajense Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambaye amekuwa kipofu kwa miaka 10, amepona na kumkataa mkewe kwa kile alichoeleza kuwa amezeeka sana.

Sikazwa ambaye kwa miaka 10 aliyokuwa kipofu alikuwa akihudumiwa na mkewe, Evelanda Sikazwa na alipona baada ya kutibiwa na madaktari bingwa wa macho kutoka Ujerumani waliokuwa wakitoa huduma mkoani kwa kujitolea.

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu mkasa wa kumkataa mkewe kabla ya kushauriawa na ndugu zake amrejee, Sikazwa alisema alipata hali ya upofu miaka 10 iliyopita hadi hivi karibuni alipopelekwa kwa madaktari hao kutibiwa.

“Baada ya kusikia kuna madaktari bingwa wa macho, binti yangu anayeishi Kijiji cha Kakese alinifuata na kuniomba twende tukawaone madaktari…nilimkubalia na matunda yake nimeyaona.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji wa macho nilifungwa bandeji machoni na kushauriwa na daktari nisizifungue kwa muda wa siku mbili.“Baada ya siku mbili nilirudi tena kwa madaktari, mmoja wao alinifungua hakika sikuamini kile kilichotokea, kwani nilianza kuona tena baada ya miaka 10 kupita,” alisema Sikazwa.

Alisema aliporejea nyumbani kwake alilakiwa na familia yake kwa furaha na kutambulishwa kwa mkewe Evelanda lakini alishindwa kumtambua na kwamba alimkataa kwa sababu alimuona ni mzee sana.

“Miaka yote 10 niliyokuwa nimepofuka mke wangu, Evelanda alikuwa akinihudumia, siku macho yangu yalipopata nuru na kuanza kuona tena sikumtambua kwa kuwa nilimwona amezeeka tofauti na nilivyokuwa nikimwona kabla ya kuwa kipofu.

“Hata hivyo, baada ya kushauriwa na ndugu zangu kuwa Evelanda ndiye mke wangu wa ndoa, niliafiki na kukubali kuendelea kuishi naye.

Siyo utani, heri mtu awe kiziwi lakini si kuwa kipofu, mpaka nilishamsahau mke wangu aliyekuwa akinihudumia hadi unyumba kwa kipindi chote cha miaka kumi bila kunung’unika, alinivumilia kwa kipindi chote hicho,” alisema Sikazwa. Akizungumzia historia ya ndoa yake, Sikazwa alisema alimuoa Evelanda mwaka 1959 katika Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga, Parokia ya Chala wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Alisema tangu alipoanza kuona tena, anazurura katika mitaa ya mji wa Mpanda akishangaa maendeleo makubwa yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na majengo mazuri na barabara nyingi zilizojengwa kwa kiwango cha lami.

Sikazwa alisema hivi sasa ratiba yake ya kila siku akiamka asubuhi anakunywa chai kisha anaingia mitaani kuangalia uzuri wa mji na kusalimiana na ndugu, jamaa na marafiki zake ambao siku zote alikuwa na hamu ya kuwaona.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.