Cristiano Ronaldo hatarini kufungiwa tena

Mtanzania - - Mbele - MADRID, HISPANIA

MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, anaweza kukutana na adhabu kali kutoka kwa Chama cha Soka cha nchini Hispania, baada ya kudaiwa kumfanyia madhambi kwa makusudi mchezaji wa Girona, Pere Pons, katika mchezo uliochezwa juzi jijini Katalunya, Hispania.

Katika mchezo huo, Madrid ilifungwa mabao 2-1 huku Ronaldo akionekana kushindwa kuisaidia timu yake ambayo kwa sasa ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 20, ambapo tofauti ya point nane dhidi ya vinara Barcelona katika msimamo wa Ligi Kuu Hispania.

Ronaldo ambaye amekuwa hasimu mkubwa wa mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi, alidaiwa kutumia mkono wake wa kulia kumkwaruza usoni mchezaji huyo wakati wakigombea mpira.

Mchezaji huyo bora wa dunia mwanzoni mwa msimu huu alifungiwa michezo mitano na kukosa michezo minne ya Ligi Kuu ‘La Liga’ baada ya kudaiwa kumsukuma mwamuzi.

Katika mchezo huo, mbali na Ronaldo kufanya vibaya, pia Mfaransa Karim Benzema hakuwa katika kiwango chake bora.

Mfaransa huyo alishindwa kuisaidia timu yake kupata ushindi katika mchezo huo na kujikuta katika wakati mgumu.

Kocha wa timu hiyo, Zinedine Zidane, alisisitiza kwamba hana hofu na kikosi chake kushindwa kupata ushindi katika mchezo huo.

“Tunafahamu tunaweza kubadili upepo na mambo yakawa safi, tunaweza kuwa na siku njema hapo baadaye na wapinzani wetu wakapoteza pointi katika msimu huu.

“Hakuna jambo tunaloweza kulifanya kwa sasa na tunafahamu muda wowote kwa sasa mambo yanaweza kubadilika, safari bado ndefu hivyo hatuna hofu na jambo lolote,” alisema Zidane.

Wakati huo huo, kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde, alimsifia Lionel Messi baada ya nyota huyo kuisaidia timu yake kushinda baada ya mapambano makali dhidi ya Athletic Bilbao.

Messi alifunga bao dakika ya 36 kabla ya Paulinho kukamilisha ushindi wa 2-0 kwa Barca ambao walikuwa katika wakati mgumu dhidi ya wapinzani wao hao Jumamosi iliyopita.

Mwargentina huyo alimpasia Jordi Alba chini kushoto kabla ya kuwahi mbele na kupokea pasi kufunga goli lake la 12 La Liga msimu huu.

Valverde hakuweza kuzuia furaha yake kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ambaye amefunga mabao 16 katika mechi 15 kwenye michuano yote msimu huu.

“Messi angeweza kufunga bao jingine kama asingegonga mwamba, lakini amekuwa mtu wa maajabu,” alisema Valverde.

“Nyota huyo anaweza kufanya tofauti muda wowote. Lilikuwa bao safi sana.

“Tuna bahati kubwa sana kuwa na mchezaji bora duniani pamoja nasi.”

Barca wapo kileleni kwa tofauti ya pointi nne La Liga baada ya kushinda mechi nane kati ya 10 za mwanzo, wakiruhusu magoli matatu tu.

Valverde amepata faraja ya moyo baada ya kuchukua pointi tatu dhidi ya klabu ambayo amewahi kuichezea na kuifundisha pia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.