Wairani 10 kortini kwa kusafirisha heroin

Mtanzania - - Habari - Na KULWA MZEE

SERIKALI imewafikisha mahakamani raia 10 wa Iran na Watanzania wawili wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kusafirisha dawa mbalimbali za madawa ya kulevya zikiwamo kilo 111.02 za heroin.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa alidai kwamba washtakiwa walikutwa katika Ukanda wa Bahari ya Hindi upande wa Tanzania.

Washtakiwa ni Nabibakshsh Bibarde, Mohammed Dorzade, Abdallah Sahib, Ubeidulla Abdi, Naim Ishaqa, Moslem Amiree, Rashid Badfar, Omary Ayoub, Tahir Mubarak, Abdulmajid Asqan, Ally Abdallah na Juma Juma.

Kishenyi alidai Oktoba 25, mwaka huu katika ukanda huo wa Bahari ya Hindi upande wa Tanzania, washtakiwa walisafirisha kilo 111.02 za heroin.

Inadaiwa siku hiyo hiyo washtakiwa hao pia walikutwa wakisafirisha gramu 235.78 za bangi.

Kishenyi alidai siku hiyo washtakiwa hao walisafirisha mchanganyiko wa bangi na kuberi zenye uzito wa kilo 3.34.

Washtakiwa walikuwa wakitafsiriwa lugha ya Kiswahili kwenda Kiirani na mkalimani Meja Ndakeye (45).

Baada ya kusomewa mashtaka hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Upande wa Mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika na washtakiwa walipelekwa rumande hadi Novemba 13, 2017 kesi yao itakapotajwa tena.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.