Muhimbili yatoa ufafanuzi ndugu kusukuma vitanda

Mtanzania - - Habari - Na VERONICA ROMWALD

BAADHI ya ndugu wa wagonjwa wanaokwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamelalamikia kuachiwa wasukume vitanda vya wagonjwa wao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa ndugu wenye wagonjwa wanaohudumiwa hospitalini hapo (jina linahifadhiwa kwa sababu maalumu), alisema ni jambo la kawaida sasa ndugu wa wagonjwa kulazimika kusukuma kitanda cha mgonjwa kwenda kwenye vipimo na hata wodini kutoka mapokezi.

“Ni changamoto kwa kweli, mimi nimepeleka mgonjwa wangu atibiwe, lakini tena unalazimika kusukuma kitanda chake hadi kwenye vipimo na wodini, kwakuwa wengine hatujazoea kufanya kazi hiyo, tunagongesha kitanda kwenye kuta za hospitali na kuleta usumbufu kwa mgonjwa wakati jukumu hilo linajulikana wazi ni la wahudumu wa afya ambao wamesomea kazi hiyo,” alisema. MTANZANIA lilipomtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha, alikiri kuwapo kwa hali hiyo ambayo ilipaswa kufanywa na watoa huduma.

Hata hivyo, alisema si kosa ndugu wa mgonjwa kushirikiana na mhudumu kumpeleka mgonjwa husika kwenye vipimo au wodini.

“Ni jukumu letu, lakini pamoja na hayo, ikumbukwe kuwa huduma ya tiba ni huduma shirikishi, hivyo ndugu wa mgonjwa ana wajibu wa kusaidia.

“Idara ya Magonjwa ya Dharura inapokea wastani wa wagonjwa 200 hadi 250 kwa siku, ikitokea kuna wagonjwa 50 kwa wakati mmoja wanahitaji kwenda kwenye vipimo na wengine wodini kama kuna wahudumu 10 wakati huo, ina maana kwamba wagonjwa 10 wataondoka kwa wakati mmoja na wahudumu kwenye vipimo ndipo warudi kuchukua wagonjwa wengine.

“Hapa lazima ndugu watalalamika kuwa wagonjwa wao wamechelewa kuhudumiwa kwa kukaa muda mrefu kusubiri wahudumu wa kuwapeleka kwenye vipimo au wodini.

“Ndiyo maana ndugu wengine wanapokuja na wagonjwa wao wanaona kwa hiari yao kushirikiana na watoa huduma katika kumhudumia ndugu yao.

“Aidha ni kitu cha kawaida ndugu wengi wenye wagonjwa wodini kuomba kukaa na wagonjwa wao wodini ili kuwapa usaidizi zaidi,” alibainisha Eligaesha.

Alisema pamoja na kwamba kuna upungufu wa watoa huduma, haimaanishi kuwa jukumu la tiba shirikishi linaondoka.

“Litakuwepo na litaendelea kuwepo, kwa sababu kwa mfano kule kwenye Jengo la Wagonjwa wa Nje (New OPD) lililopo mkabala na Jengo la Wazazi, kwa siku hupokea wagonjwa wapatao 700, sasa ikitokea kwa mfano siku hiyo wakapokea wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura 100, maana yake tutatakiwa kutafuta wahudumu 100 kusaidia wagonjwa hao, unaona wazi ni muhimu kushirikiana kati ya wahudumu na ndugu,” alisisitiza.

PICHA: AMON MTEGA

SHIDA YA MAJI: Wanafunzi wa Sekondari ya Mgomba, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wakichota maji mtoni kutokana na tatizo la uhaba wa maji baada ya bomba inalohudumia shule hiyo kuharibika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.