Operesheni tudhibiti uchafu ije na mabadiliko

Mtanzania - - Tahariri -

JIJI la Dar es Salaam linasifika kuwa na shughuli nyingi za kijamii ambazo husababisha uzalishaji takataka kuwa juu. Kutokana na hali hiyo, kumekuwapo na milipuko ya magonjwa kama kipindupindu ambacho huua watu wengi na kuwaacha wengine wakiwa hoi.

Hii yote hutokana na kukithiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali, yakiwamo ya makazi na viwanda. Katika eneo la makazi, tumekuwa tukishuhudia kuwapo na malundo ya takataka na maji machafu, ambayo ni hatarishi kwa afya za binadamu.

Leo tumelazimika kusema haya, baada ya Serikali kuwataka wananchi kuzingatia usafi kwa kusafisha mitaro na kuzibua maji yaliyopo katika mito ili kuepukana na adha ya mafuriko inayosababishwa na kuwapo takataka ngumu zinazozuia utiririkaji wa maji kwa urahisi.

Ili kuonyesha imedhamiria kupambana na hali hiyo, Serikali imekuja na ‘Operesheni Tudhibiti Uchafuzi wa Mazingira Tusalimike’, ambayo inatarajia kuanza kesho nchi nzima.

Operesheni hiyo, imezinduliwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, ambaye alisema ili jamii ibaki salama katika mazingira yao, lazima kuzingatia dhana ya usafi.

Alisema kumekuwa na tabia ya wananchi kutupa takataka ngumu katika mitaro na kuiziba jambo ambalo linasababisha mifereji ya maji, mitaro na mito kushindwa kupitisha maji na kusababisha mafuriko katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.

Hakuna ubishi kwamba Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na maeneo mengi kugeuka kuwa hatarishi kwa uhai wa wananchi, hasa katika vipindi vya mvua kama vile Manzese, Kwa Mtogole, Buguruni na mengine.

Tunasema hivyo, kwa sababu kumekuwapo na tabia ya wananchi kutoshehimu miundombinu iliyopo, jambo ambalo kila mwaka tumeshuhudia majanga makubwa ikiwamo na wananchi kupoteza uhai.

Tunakupongeza Waziri Lugola kwa kuona hilo, lakini tunakushauri jambo hili lisiwe la zimamoto kama ambavyo wamekuwa watangulizi wengi wakianzisha kisha kuishia njiani.

Tunaamini Waziri Lugola, kwa jambo hili utakuwa umejipanga vya kutosha kutoa elimu maeneo yote ambayo yamekuwa ni tatizo. Tunasema haya yote yatawezekana kama Serikali itajipanga vizuri kuanzia ngazi ya mtaa kufanya kazi ya kuwaelimisha wananchi na kutoa vitendea kazi, ikiwamo magari ya kuzolea taka. Siku zote kwa kuwa viongozi wa ngazi za chini ndiyo wanaishi na jamii, lazima waonyeshe kuwa wapo na wanaweza kusimamia mambo haya.

Halmashauri zote za majiji, manispaa na miji, zijipange kuwashirikisha wananchi kwa kila hatua ili mwisho wa siku kuondokana na adha hii.

Haiwezekani viongozi wa ngazi za wilaya na mikoa waliokabidhiwa majukumu haya, wanakuwa watu wa kushinda wamejifungia ofisini tu, badala ya kwenda kwa wananchi kutoa elimu inayotakiwa.

Sisi MTANZANIA, tunasema Waziri Lugola kwa kuwa umeanzisha kitu cha msingi, hakikisha unakisimamia ipasavyo na kisiwe nguvu ya soda.

Tunataka kuona tatizo la uchafu ambalo limekuwa sugu katika miji kama Dar es Salaam, linapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili tuwe na miji safi na yenye kukidhi viwango.

Tunamalizia kwa kusema Waziri Lugola huu ni mtihani wako wa kwanza tangu ulipopewa nafasi hii, hivyo onyesha unaweza, kataa uchafu wa Dar es Salaam ambao miaka nenda rudi umeshindwa kufutika machoni mwa watu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.