Serikali ihamasishe wakulima wa mihogo

Mtanzania - - Tahariri - Na SHERMARX NGAHEMERA

SUALA la mahitaji ya mhogo kutoka China lisiachiwe watendaji wa Serikali wasio na uchungu wa nchi hii bali lishikwe na wale wenye uzalendo na uchungu wa nchi hii ambayo pamoja na kuwa na rasilimali lukuki nyingi bado inaendelea kuwa masikini.

Kutokana na habari kuwa zinatakiwa tani milioni 1.2 za mihogo kule China, ni habari njema sana kama Balozi Mbelwa Kairuki anavyodai na kuthibitisha kuwa zinahitajika kule China na kushangaa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inajivuta kutekeleza maombi hayo badala ya kuwasiliana na wahitaji na kupanga mikakati ya utekelezaji.

Mahitaji hayo ni makubwa kwa kiasi chochote cha biashara ya kimataifa na thamani yake jumla ni biashara ya kiasi cha dola milioni 90 kwa mwaka ambayo ni sawa na Sh bilioni 190. Kiuzalishaji utaona kuwa tuna uwezo wa kufikia uzalishaji unaotakiwa na kupata makopa hayo.

Wachina wanahitaji makopa ya muhogo kwa ajili ya kutengeneza kama chagizo cha mafuta ya kuendeshea magari na mitambo kwa kuchanganya na ethanol na hivyo kilishi mwendo hicho kutumika Uchina ili iweze kufikia lengo la kupunguza uzalishaji wake wa gesi ukaa kwa kiwango cha asilimia 20 kufikia 2020 na hii maana yake ni ‘oda’ ya kudumu ya kupeleka mihogo China.

Uzalishaji wa mihogo si kazi sana na mahitaji yake ya ardhi si makubwa sana, kwani huota katika maeneo ambayo hata yasiyo na ardhi nzuri kwa kilimo kingi na maeneo makame. Serikali yetu nayo inayo magereza ambayo wafungwa wanakaa bure na hivyo basi ingekuwa mwafaka kuwa wangetumika vilivyo kuzalisha mihogo ambayo ingeuzwa China na kwingineko kwani mahitaji yanazidi kukua. Hata kule Kilimanjaro ambako wanadai hawali mihogo kwani wakila huwadhuru, huu ungekuwa wakati mzuri kwao kulima zao la mihogo kama la kibiashara ili lipelekwe China.

Mahali kwenye ardhi duni kama Wilaya ya Hai nao wangepanda mihogo kwani tani moja ya mihogo ni dola 36 hadi 75 au shilingi 165/kwa kilo kwa habari toka Shirika la Chakula la Kimataifa (FAO), bei hiyo hufuatana ubora wa mihogo yenyewe ukizingatia matumizi yake.

Tuseme mihogo inahitajika sana ulimwenguni sasa kwa mahitaji ya viwanda kama nishati, gundi au wanga (starch) kuimarisha mazao mbalimbali ya viwanda ikiwamo utengenezaji vifungashio na uimarishaji wa karatasi za aina mbalimbali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.