Kamati yataka utata Rock City utatuliwe

Mtanzania - - Kanda - Na PETER FABIAN

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeiagiza bodi ya kampuni ya ubia ya uendeshaji wa jengo la kitegauchumi la Rock City Mall kumaliza utata wa gharama za ujenzi na mgawanyo wa hisa.

Agizo hilo lilitolewa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Josson Rweikiza, katika ziara ya kamati hiyo juzi.

Jengo hilo linaendeshwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Pensheni wa LAPF na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Rweikiza alisema mradi huo ni kitegauchumi kizuri na kikubwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Alisema kwa sababu hiyo ni muhimu jingo hilo likaendelea kutangazwa ili kuvutia wawekezaji na wapangaji na kulitunza liendelee kuchangia pato la taifa na kuongeza ajira kwa wananchi.

Meneja wa Kampuni inayosimamia na kuendesha jengo hilo (MCCCCL), Annette Shoo, alisema jengo hilo limeingiza Sh bilioni 2.9 na kutengeneza ajira 600.

Alisema vilevile limepandisha thamani ya ardhi inayolizunguka na kuibua biashara mpya kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

“Hadi Oktoba mwaka huu asilimia 70 ya jengo hili lenye ukubwa wa mita za mraba 21,081.74 imepangishwa ambayo ni mita za mraba 14.771.

“Na mapato ya kodi ya pango kwa mwaka mmoja uliopita kufikia Septemba, mwaka huu ni Sh bilioni 2.9. “Tunatarajia ajira zaidi na mapato kuongezeka kufikia Sh bilioni 4.2 iwapo jengo lote litapangishwa kwa sababu hadi sasa biashara zilizopo ndani zimeongezeka na wananchi wapatao 600 wamepata ajira za moja kwa moja na zisizo rasmi,” alisema Shoo.

Alisema bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za uendeshaji ikiwamo kasi ndogo ya kupata wapangaji ndani ya jengo.

Alisema hiyo ni kutokana na ari ndogo ya wawekezaji kwa sababu mfumo wa kufanya biashara ndani ya jengo hilo ni mgeni katika Kanda ya Ziwa.

UHAKIKI: Meneja wa Kampuni ya ubia baina ya Mfuko wa Pensheni wa LAPF na Halmashauri ya Jiji la Mwanza (MCCCCL), inayosimamia uendeshaji mradi wa Rock City Mall, Annette Shoo, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na...

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.