CWT watishia kutangaza mgogoro na mwajiri

Mtanzania - - Kanda - Na RAPHAEL OKELLO

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Bunda kimeiomba Serikali kuhakikisha kinalipa madeni na na stahiki za walimu mapema.

Kimesema uvumilivu una mwisho ikizingatiwai hali inazidi kuwa mbaya na hivyo kinaweza kutangaza mgogoro na mwajiri.

Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Bunda, Mongson Kabeho alikuwa akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho juzi.

Alisema walimu wamekuwa wakielezwa kuwa siyo wazalendo kila wanapodai madeni yao ili kuwakwamisha wasilipwe.

Kabeho aliwaonya watendaji wa serikali kuacha tabia hiyo kwa kuwa chombo pekee chenye mamlaka ya kusimamisha mshahara wa walimu ni Tume ya Utumishi wa Umma (TSC) pekee.

Alisema kwa kipindi cha miaka miwili, walimu wamekuwa kimya wakisubiri ahadi ya serikali ya kutekeleza madai yao jambo ambalo limekuwa ndoto.

Alisema endapo serikali itaendelea kutowalipa madai yao watatangaza migogoro na serikali.

“Tunapojitokeza kudai serikali inatuambia tuwe wazalendo, tumekuwa wazalendo wa kutosha na itafika hatua tutatangaza migogoro dhidi ya serikali,” alisema Kabeho.

Alitaja baadhi ya madai hayo kuwa ni walimu wenye sifa kutopandishwa daraja, madeni ya malimbikizo ya mishahara, nyongeza ya mishahara, deni ya Sh milioni 45 ya walimu waliosimamia mtihani wa darasa la nne mwaka 2015. Madai mengine ni serikali kuamua kutoa adhabu za udhalilishaji kwa baadhi ya walimu bila kufuata sheria na kanuni za utumishi, kutokana na baadhi ya waajiri kutoelewa vema sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Walimu waliunga mkono hoja hizo na kuwataka viongozi wao kuibana serikali iwatendee haki kwa kile walichodai kuwa mazingira ya kazi yanawakatisha tamaa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.