Ilemela wakamilisha kupima viwanja shirikishi 14,900

Mtanzania - - Kanda - Na PETER FABIAN

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela imejipanga kuboresha makazi kwa kupima viwanja 14,905 kati ya 28,815 katika upimaji shirikishi na urasimishaji makazi ambao ulitolewa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga alikuwa akitoa taarifa kwa wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Alisema hadi kufikia Juni mwaka huu viwanja 14,905 vilikuwa vimekwisha kupimwa na kutolewa hatimiliki 2,067 ambazo ziliandaliwa na maombi yake kuwasilishwa kwa Kamishina Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa.

Wanga alisema viwanja 13,910 viko kwenye hatua mbalimbali za upimaji katika mitaa ya kata 19 ambazo hati zake 1,640 zinaendelea kuandaliwa na wataalamu wa manispaa.

“Changamoto ya upimaji shirikishi ni mwitikio mdogo wa wananchi kuchangia gharama za upimaji na kuandaliwa kwa hatimilki.

“Agosti mwaka huu wananchi pekee waliolipia ni 101, wananchi pia wanakosa nyaraka muhimu za kukamilishia hatimilki ikiwamo uthibitisho wa uraia,”alisema.

Wanga alisema baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kuachia maeneo yao kwa ajili ya kutengwa kujengwa majengo na sehemu za viwanja vya michezo na wazi na huduma za jamii.

Alisema pia wapo wananchi wengine waliovamia maeneo yaliyotengwa na kupimwa kwa huduma za jamii.

“Nimekuwa nikiongozana na wakuu wa idara ambao ni wataalamu wa halmashauri kuhimiza wananchi kulipia gharama za upimaji shirikishi na umilikishaji tukishirikiana na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula (CCM) na madiwani kwenye kata zao katika mikutano ya hadhara,”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.