ASPA: Watafiti wekezeni utafiti kwa punda

Mtanzania - - Kanda - Na ELIYA MBONEA

WATAFITI wa mifugo nchini, wametakiwa kuwekeza tafiti zao kwa punda, kwa kuwa inakadiriwa zaidi ya punda 500,000 kati ya milioni 1.5 waliopo nchini, wanakabiliwa na magonjwa ya ngozi.

Hayo yalielezwa juzi mjini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Arusha Society for the Protection of Animals’ (ASPA), Livingstone Masija, alipokuwa akielezea juu ya umuhimu wa kumtunza mnyama huyo.

Masija alisema kwamba, kutokana na watafiti wengi nchini kutowekeza tafiti zao kwa punda, kumesababisha kutokuwapo kwa takwimu za kiuchumi, kijamii na kiafya kwa mnyama huyo katika maeneo mengi hususani vijijini.

“Punda hapewi umuhimu sana na watafiti wengi, pengine kwa vile amekuwa anaonekana hana thamani katika jamii.

“Lakini, pia utafiti kuhusiana na maradhi yao hauonekani kuwa na umuhimu, jambo ambalo watafiti wanatakiwa kuachana nalo.

“Yaani, zaidi ya asilimia 90 ya punda walioko nchini, wamekuwa wakitumika mashambani, kubeba kuni, kubeba maji, kuvuta mizigo mikubwa kwenye mikokoteni na katika shughuli zingine za kijamii,” alisema Masija.

Akifafanua umuhimu wa utunzaji wanyama hao wanaotumika kama nguvu kazi katika maeneo mengi vijijini, Masija alisema kuna haja kwa jamii kuwatunza dhidi ya magonjwa na maambukizi mengine badala ya kuwatelekeza. “Ngozi au mwili wa mnyama huyu unaweza kuathirika na vimelea vya magonjwa mbalimbali vikiwamo bakteria, virusi, fangasi, kupe, chawa, viroboto, utitiri na inzi.

“Vimelea hivi husababisha madhara kama kujikuna, kupukutika manyoya, vidonda na magonjwa kama pepopunda na pia wadudu kama kupe wanaokuwa katika ngozi ya mnyama huyo, hueneza magonjwa ya ndigana kali na ndigana baridi,” alisema.

PICHA: WIZARA

TUMEWAKAMATA: Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akiangalia ng’ombe aina ya Nyankole kutoka nchini Rwanda, waliovamia katika Kijiji cha Kakere, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma juzi, wakisubiri kukamilika kwa taratibu za mahakama kupigwa mnada.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.