Viongozi wa mila Monduli wampongeza JPM

Mtanzania - - Kanda - Na ABRAHAM GWANDU

VIONGOZI wa kimila wa kabila la Wamasai waitwao Laigwanan wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha, wamempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa jinsi anavyotaka rasilimali za nchi ziwanufaishe Watanzania.

Wazee hao walitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wilayani Monduli, baada ya kumalizika kwa kikao chao cha kimila kilichofanyika chini ya mti maarufu uitwao Olopon.

Katika mti huo ndipo Waziri Mkuu wa Zamani, Hayati Edward Sokoine, aliposimikiwa kuwa kiongozi wa mila wa kabila hilo.

Mwenyekiti wa viongozi hao, Ngiboli Ngilepoi, alisema wao kama viongozi wa mila, wanampongeza Rais Dk. Magufuli kwa jinsi anavyohakikisha rasilimali za Taifa zinarudi mikononi mwa wananchi.

“Sisi kama wazee hatutakuwa nyuma katika juhudi za kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwa amesaidia kupambana na wezi wa rasilimali za Taifa,” alisema Ngilepoi.

Njokota Lami ambaye pia ni miongoni mwa wazee wa mila, alisema Rais Dk. Magufuli anastahili kupongezwa kwa sababu anajitahidi kuwasimamia watendaji walio chini yake wakiwamo mawaziri na viongozi mbalimbali.

“Hata uamuzi uliofanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, wa kurejeshwa kwa mifugo ya wakazi wa Loliondo iliyokamatwa wilayani Serengeti, ni uamuzi wa kujali masilahi ya wanyonge.

Naye Loota Sanare, alisema yeye na wenzake walilazimika kukutana chini ya mti huo kama sehemu ya kuutambua na kwa kuwa maamuzi mengi katika jamii ya Kimasai, hufanywa chini ya mti huo.

“Kwa hiyo, sisi kama viongozi wa kimila na wafugaji wa kimasai, tunampongeza Rais Magufuli kwa sababu anawajali Watanzania.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.