China yahitaji mihogo tani milioni 1.2

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Na MWANDISHI WETU - CHINA

TANZANIA pamoja na kuwa na maajabu ya wanyama wake na ndege na viumbe vingine vyenye uhai, Taifa hili lina maofisa serikalini ambao hawajali wala hawasikii vilio vya watu.

Habari kutoka China zinaonesha kuwa Wizara yetu ya kilimo haitaki kushughulikia mahitaji ya China ya kuuziwa mihogo mikavu tani 100,000 kila mwezi na kufanya jumla ya tani 1,200,000 yaani tani milioni moja na laki mbili kwa mwaka.

Hayo yamethibitika katika kikao cha pamoja cha Jukwaa la China na Tanzania kujadili masuala ya biashara na uchumi ambapo Watanzania walilaumiwa kwa kutoshughulikia mambo yanavyotakikana na kujivuta miguu kutekeleza makubaliano ya biashara.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, ameiomba Wizara ya Kilimo kutumia fursa iliyotolewa kwa nchi na wataalamu wa Kichina ili nchi hiyo iuziwe mihogo mikavu kwa matumizi yao ya nishati.

Balozi Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao

cha sita baina ya nchi mbili hizo mjini Guangzhou, Kusini Magharibi ya China kwa wajumbe zaidi ya 300 waliohudhuria hapo kongamano hilo. Kwa maelezo yake Balozi Kairuki ni kuwa China inataka kupunguza matumizi yake ya petroli na dizeli kwa asilimia 20 hadi kufikia mwaka 2020 na hivyo kuhitaji mihogo hiyo ili kutengeneza nishati ya mchanganyiko na ‘ethanol’ kuendeshea magari na hivyo kupunguza uchafuzi wa hewa na kufikia mahitaji ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya hali ya nchi.

“Tumepata fursa hii adhimu na tunaonekana kushindwa kuitumia vilivyo kwani toka mkataba ulivyosainiwa na China mwaka jana 2016, hajaona wala kusikia Wizara imewaona wakulima na kuwashauri walime zao hili ambalo ni rahisi na halihitaji maji mengi wala mbolea pamoja na kuhimili ukame,” anasema.

Anasema Wizara iwashauri vilivyo wakulima walime mihogo ili nchi iweze kutekeleza mkataba huo ambao ni wa fedha nyingi sana kwa uchumi wa taifa.

Akizungumzia kuhusu fursa nyingine zilizopo kati ya nchi mbili hizi ni uwepo wa mfuko wa maendeleo unaojulikana kama ‘China Africa Development Fund (CADF)’ ambao inakuza uwezo wa bara hili katika masoko mbalimbali. Anasema mfuko huo una mtaji wa dola bilioni 5 unaokopesha wafanyabiashara wa Afrika ambao wanafanya biashara na ubia na watu wa China.

Alisema Tanzania imeshafaidika na mfuko huo kwani kuna takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya dola milioni 700 zimeshatumika na Watanzania na kuwekezwa kwani Wachina wako tayari wakati wote na kushauri Watanzania tugangamale vilivyo.

Du Chwan, Mkurugenzi wa Kampuni inayoagiza mihogo duniani kote, aliwahakikishia wajumbe kuwa kampuni yake mwaka jana pekee iliagiza zaidi ya tani milioni kumi za mihogo mikavu na upatikanaji wa tani 100,000 kwa mwezi ni stahiki.

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda na Uwekezaji, Prof Adolf Mkenda, alisisitiza kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili hizi na kutaka wananchi wake kushirikiana na kuwakaribisha Wachina kuja kuwekeza Tanzania.

Alisema Tanzania ina nafasi nzuri kwa uwekezaji ukizingatia nafasi yake ya kimkakati ya kijiografia, amani iliyotandawaa na rekodi nzuri inayoongoza ya kuvutia wawekezaji wa moja kwa moja (FDI) katika Afrika Mashariki.

Profesa Mkenda amesema Tanzania inakaribisha wawekezaji katika kuongeza thamani mazao yake na kupata vivutio mbalimbali.

Aliyekuwa Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Yuqing, alitoa ushuhuda juu ya hali nzuri ya uwekezaji nchini Tanzania.

Alisema Tanzania ina uchumi ambao unakua kwa asilimia 7, hali imara kisiasa, rasilimali za kila aina za kutosha, mahusiano mazuri na nchi nyingine duniani na ardhi nzuri kwa kilimo ambavyo vyote ni vitu vizuri kuvutia uwekezaji.

Alikomelea kwa kusema kuwa kutokana na maboresho yanayofanyika katika miundombinu nchini, itasaidia sana kupeleka mbele Taifa na kuwa sumaku ya kuvutia wawekezaji.

Dk. Lu aliiomba Serikali ya Tanzania kuwa na sera madhubuti za uwekezaji na kupunguza urasimu katika kushughulikia mambo mbalimbali ya vibali vya Serikali ili kuharakisha ufanyaji maamuzi.

Anasema China imewekeza zaidi ya dola bilioni 3.6 na kusifu juhudi za Rais John Magufuli katika kupambana na rushwa na uhalifu.

Tayari Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeanzisha mpango wa jopo la kitaifa la watu wanaohusika na kufanya maamuzi ya uwekezaji ili kupunguza muda wa kufanya maamuzi na kupunguza gharama za kuhangaika kwenda katika ofisi mbalimbali na badala yake maamuzi yatafanyika mahala pamoja katika ofisi ya TIC.

Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe, aliwahi kusema hata ‘land bank’ ya Taifa itamilikiwa na taasisi yake na vile vile itahusika na ukusanyaji wa ada mbalimbali za malipo kwa taasisi za umma na halafu kuzigawa kwa taasisi husika.

Taasisi mujarabu kwa uwekezaji ni TFDA, TBS, TEMDO, NIMRI, SIDO, NEMC na Tanzania Atomic Energy Commission.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki.

Mihogo hupatikana kwa wingi karibu mikoa yote Tanzania

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.