Tumbi Sekondari kinara shindano Elimu ya Kodi

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Na KOKU DAVID - DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imeazimia kufikisha elimu ya kodi kuanzia kwa watoto shuleni hadi kwa wadau mbalimbali ambao kwa mujibu wa sheria wanastahili kulipa kodi.

Katika kuhakikisha azma hiyo inatimia, TRA imekuwa ikiendesha mashindano ya klabu za kodi kwa shule za sekondari nchini.

Shule mbalimbali za sekondari zimekuwa zikishiriki katika mashindano hayo ambayo shule inayofanya vizuri hupata zawadi.

Hivi karibuni katika Chuo cha Kodi (ITA) kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, TRA ilishindanisha shule za sekondari 45 kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ili kuweza kuona uelewa wao katika masuala mbalimbali ya kodi.

Shule mbalimbali za sekondari zimekuwa zikishiriki katika mashindano hayo ambayo shule inayofanya vizuri hupata zawadi.

Katika mashindano hayo, Shule ya Sekondari Tumbi iliibuka mshindi wa jumla katika maswali na majibu, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Shule ya Sekondari Minaki na nafasi ya tatu ikienda kwa Sekondari ya Maarifa.

Pia katika uwasilishaji mada vizuri, Shule ya Sekondari ya Misitu ndiyo iliyoibuka mshindi huku, Shule ya Sekondari ya Pugu ilifanya vizuri katika shindano la ukusanyaji risiti zilizotokana na mashine za kielektroniki za EFD ambazo walizipata kutokana na bidhaa walizonunua madukani.

Kabla ya fainali ya mashindano hayo, maofisa wa TRA hutembelea katika shule mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi kwa wanafunzi wote ambao ni wanachama wa klabu za kodi.

Baada ya mafunzo hayo kwa wanafunzi, katika maadhimisho ya siku ya mlipakodi, TRA huwashindanisha na shule itakayofanya vizuri hupata zawadi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, anasema lengo la kuanzishwa kwa mashindano ya klabu za kodi katika shule za sekondari ni kuhamashisha ulipaji wa kodi katika jamii.

Anasema kwa kuwajenga wanafunzi katika kuwapa elimu ya kodi, kutasaidia ongezeko la ulipaji wa kodi kwa wananchi lakini pia kuandaa wataalamu wa baadaye.

Anasema kuwajenga vijana katika umri mdogo hadi watakapokuwa watu wazima watakuwa na uelewa mkubwa wa umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi na hivyo kuitazama kodi katika mfumo bora zaidi na kuikubali bila shuruti.

Kichere anasema kuwa kutokana na mafunzo waliyopata kutoka kwa maofisa wa TRA, wanafunzi hao wameonyesha uwezo mkubwa katika uelewa wa masuala ya kodi ambayo kwa miaka ya baadaye itakuwa ni faida kwa nchi.

Anasema kutokana na mada zilizokuwa zikiwasilishwa na washiriki wa mashindano hayo, imetoa hamasa kubwa kwa TRA kuhakikisha wanachama wa klabu za kodi wanaongezeka nchi nzima.

Anasema sambamba na kuongeza klabu za kodi, pia itaongeza utayari wa ulipaji kodi kwa wananchi kutokana na kuwa wanafunzi hao watakuwa wakihamasisha ulipaji kodi hasa kwa kudai risiti kila baada ya kuhudumiwa na mfanyabiashara kutokana na bidhaa zitakazokuwa zimenunuliwa.

Anaongeza kuwa kudai risiti kila baada ya kuhudumiwa kutasaidia kuongezeka kwa kodi ya ongezeko la thamani.

Anasema kushirikisha wanafunzi katika masuala ya kodi ni kuongeza jeshi ambalo litaiwezesha TRA kufikia malengo yake katika suala zima la ukusanyaji mapato kama ambavyo Serikali imeitaka.

Anasema mashindano hayo yatakuwa endelevu na kwamba kuwaelimisha wanafunzi kutaifanya elimu ya kodi isambae katika jamii kutokana na kuwa nao wataipeleka kwa walimu wao, wazazi, ndugu pamoja na jamii inayowazunguka.

Kichere anasema kutokana na uwezo mkubwa ulioonyeshwa na wanafunzi hao, ni dalili nzuri ya mamlaka ya mapato kufanikiwa katika malengo yake iliyojiwekea kwani inaamini kuwa inaandaa wataalamu wazuri wa kodi, ikiwa ni pamoja na walipakodi ambao watakuwa wazalendo kwa nchi yao katika miaka ya baadaye.

Anasema TRA inatoa wito kwa jamii yote kuwa wazalendo katika suala zima la ulipaji wa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Kamishna mkuu wa TRA, charles kichere

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.