Wanawake wajasiriamali wawa chachu kukuza biashara

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi -

Changamoto ni namna ya kuongeza ushiriki wa taasisi za Serikali hususani zinazohusika na uendelezaji. – Blandina Sembu

OKTOBA 26, mwaka huu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alizindua maonyesho ya wanawake wajasiriamali yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja,D ar es Salaam.

Maonyesho hayo huwakutanisha wajasiriamali wanawake kutoka sehemu mbalimbali nchini sambamba na wadau wengine muhimu kama vile benki, wakala wa taifa wa vipimo na taasisi nyingine zinazohusika moja kwa moja au kwa namna au nyingine na ujasiriamali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo ya 11 yanayofahamika kama Tamasha la Mwanamke Mjasiriamali (MOWE), Mjumbe wa tamasha hilo, Blandina Sembu, anasema tangu kuanzishwa kwa maonyesho hayo mwaka 2006 wameweza kuvutia zaidi ya wanawake wajasiriamali wapya kujitokeza kuonyesha bidhaa zao.

Kupitia maonyesho hayo vyombo mbalimbali vimeweza kuchukua changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili na kuchukua hatua stahiki kuzishughulikia, hivyo kuwasaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Blandina anasema wameweza kuunganisha wajasiriamali na watoa huduma za kifedha na zisizo za kifedha pamoja na watunga sera kwa lengo la kukuza mitaji ya wajasiriamali.

Anasema miongoni mwa taasisi zilizoweza kuunganishwa na wajasiriamali ni Brela, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambazo zimekuwa zikisaidia kutoa elimu na kuhamasisha mambo mbalimbali kama vile kurasimisha biashara, kusajili biashara na usajili wa miliki bunifu.

Anasema pia wamekuwa wakishirikiana na SIDO ambao wamekuwa wakitoa elimu juu ya matumizi ya vifungashio bora na namna ya kuviweka chapa na kutangaza biashara.

Anasema MOWE imekuwa chachu ya ukuaji wa biashara kwa kuwashawishi wanawake kutumia fursa za biashara na maliasili zinazopatikana, kubuni, kuanzisha na kuendeleza biashara nchini na kufanya bishara zenye staha na kuepuka kuwa wategemezi.

MOWE wanaiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuratibu utoaji wa vibali vya uthibitisho wa ubora wa bidhaa kwa kuwa na sehemu moja ya kutoa vibali hivyo yaani (one stop centre) tofauti na sasa ambapo hutolewa na taasisi tofauti tofauti, hali inayosababisha usumbufu na kusababisha gharama kubwa kwa wajasiriamali hao.

Wanaishauri Serikali kufufua viwanda na kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa gharama nafuu pamoja na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wanaitaka Serikali itenge maeneo maalumu ya kuzalishia bidhaa kwa wanawake hasa kwa kuzingatia kuwa wanawake wengi waliojikita kwenye sekta ya usindikaji hawana maeneo mwafaka ya kuzalishia.

Kuhamasishwa kwa matumizi ya bidhaa za asili zinazozalishwa na wajasiriamali nchini na kuanzishwa kwa kituo maalumu kitakachotumika kuonyesha bidhaa za Kitanzania nje ya nchi.

Wanaiomba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kusaidia taasisi za Serikali ziweze kushiriki kikamilifu maonyesho ya MOWE ili kusaidia kuwajengea uwezo wajasiriamali.

“Changamoto mojawapo ni namna ya kuongeza ushiriki wa taasisi za Serikali hususani zinazohusika na uendelezaji wa ujasiriamali nchini.

“Tunaomba Wizara yako isaidie kutoa hamasa kwa wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kushiriki kwenye maonyesho haya, ambapo ushiriki wao utasaidia kutoa elimu na maelezo ya kina kwa washiriki ambao wamekuwa wakiyakosa kwenye maeneo wanakotoka,” anasema Blandna.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwijage aliwataka wajasiriamali hao kuzalisha kwa wingi bidhaa wanazoona zinauzika vizuri ili waweze kupata faida; yaani waanzie sokoni.

“Hii kazi mnayofanya ya uchakataji au uongezaji thamani ndio kazi mama na muhimu katika viwanda, hivyo zalisha kwa wingi ili kupata faida. Hakuna sababu ya kuwa na aina nyingi za bidhaa, chagua moja uzalishe kwa wingi,” anasema Mwijage.

Anaahidi kuwa Serikali imejizatiti kuhakikisha inaanzisha vituo maalumu vitakavyotumiwa na wajasiriamali kuchakata bidhaa zao ili kuziongezea thamani.

Anasema tayari maagizo yamekwishatolewa kila wilaya kuhakikisha inakuwa walau na kituo kimoja cha aina hiyo ili kuwawezesha wajasiriamali hao ambao wengi wao hawana uwezo wa kununua mashine ambazo ni ghali kwa sababu huagizwa kutoka nje ya nchi.

Anasema kwa Mkoa wa Dar es Salaam vitajengwa kati ya vituo vitatu hadi vitano kwa kila wilaya na vitakuwa vikifanya kazi usiku na mchana ili kutoa fursa kwa watu wengi kuvitumia.

Anawashauri wafanyabiashara hao kutumia maonyesho hayo yaliyofikia tamati Oktoba 30, mwaka huu, kujifunza kutoka kwa wenzao mbinu mpya za kuzalisha bidhaa bora.

“Mnaweza kutumia maonyesho haya kutengeneza mtandao wa kibiashara, wewe unaweza kuwa unafanyia biashara Mwanza ukaungana na mwenzako wa Mbeya ambako kuna soko la bidhaa unayozalisha ukawa unamtumia bidhaa zako anauza naye anakutumia bidhaa zake,” anasema.

Anasema mtandao wa aina hiyo utawasaidia kufahamu wapi zinapopatikana malighafi za bei nafuu ambazo zinaweza kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo bidhaa kuwa shindani katika soko.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.