Utalii wa kitamaduni Mikumi kupunguza ujangili, kukuza uchumi

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Na LILIAN JUSTICE - MOROGORO

HIFADHI ya Taifa ya Mikumi ni miongoni mwa hifadhi za Taifa mashuhuri na kubwa nchini ambayo pia imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya matukio ya ujangili na ajali za wanyama, matukio ambayo yamewaathiri wanyama wengi wanaopatikana katika hifadhi hii, iliyoko mkoani Morogoro, ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 3,230 ambapo ilianzishwa rasmi mwaka 1964.

Hata hivyo, kwa sasa matukio hayo yameanza kuonekana kupungua, baada ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na uongozi wa hifadhi hiyo kwa kutoa elimu husika, huku ujio wa utalii wa utamaduni ulioanzishwa na wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo ukitajwa kusaidia vijana wengi kupata ajira na kuachana na ujangili wa kuua wanyama wanaopatikana hifadhini humu.

Mbali na kusaidia kutoa ajira kwa vijana na kupunguza matukio ya ujangili, utalii huo umeanzishwa katika Hifadhi za Kusini, ili kwenda sambamba na uhifadhi unaopatikana ukanda wa Kaskazini, ambao utaratibu huo walikuwa nao toka kipindi cha nyuma na kupelekea wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hizo kunufaika kiuchumi.

Aidha, upo umuhimu wa uanzishwaji wa utalii huo wa kiutamadani katika hifadhi kwani faida zake ziko wazi katika kuinua na kupunguza matukio ya ujangili katika hifadhi ya Mikumi na namna imewasaidia vijana wanaoishi katika mji huo, kuondokana na umasikini na kujiinua kiuchumi. Ingawa changamoto mbalimbali zimeendelea kuikabili hifadhi ya Mikumi.

Awali watalii waliotembelea hifadhi ya Mikumi waliweza kujionea vivutio tofauti tofauti vinavyopatikana katika hifadhi hiyo, wakiwemo wanyama wa aina mbalimbali, lakini kwa sasa umeongeza utalii mwingine wa kitamaduni, ambao nao umekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaofika katika mji wa Mikumi.

Akizungumzia jitihada hizo ambazo zinaonekana kuzaa matunda, mratibu wa utalii wa kitamaduni katika hifadhi za Kusini, Makene Ngoroma, anasema wameamua kuchukua jukumu la kuanzisha utalii huo kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo, kutokana na vijana wengi wanaoishi katika eneo hilo, kushindwa kutumia vyema uwepo wa hifadhi katika kujiingizia kipato.

Ngoroma anasema kwa hivi sasa vijana wamebadili mitizamo yao na kuanza kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kitamaduni ambazo zinawavutia wageni kununua na hivyo kujikuta wakijiongezea kipato na kuachana na kujiingiza kwenye suala la ujangili ambalo ni kosa kisheria.

Kwa upande wake Ofisa Utalii na Masoko Hifadhi ya Mikumi, Godfrey Mwakipeje, anaeleza kuwa utalii wa utamadani unakuja na bidhaa mbalimbali ambazo zinaweza kuwahamasisha watalii wanaokuja hifadhini kuja na kujionea aina mpya ya kivutio hicho katika hifadhi hizi za Ukanda wa Kusini.

Mwakipeje anasema utalii huo umeonekana kuanza kwa mafanikio makubwa kwa vijana wengi katika mji huu wa Mikumi kuanza kujiingizia kipato na kujiinua kiuchumi huku ujangili dhidi ya tembo ukipungua.

Anaeleza kuwa upekee wa hifadhi hii ni kufikika kirahisi mahali ilipo, pamoja na maeneo ya vivutio kwa kipindi chote cha mwaka, lakini hata hivyo changamoto kubwa inayoendelea kuwa tishio katika hifadhi hii, ni kuendelea kuwepo kwa vifo vya wanyama wanaogongwa na magari yanayopita katika Barabara ya Dar es Salaam –Zambia, ambayo imepita ndani ya hifadhi hiyo. Isitoshe wageni wanapata utalii wa bure kwa kupita hapo kwani huona rasilimali yetu.

Kwa takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kati ya nyumbu, swala, nyati na wanyama wengine wadogo ndio hugongwa kila siku na magari yanayopita katika barabara hiyo, hali ambayo imeathiri shughuli za uhifadhi na hata kupunguza idadi ya baadhi ya wanyama wanaopatikana hifadhini humo likiwa ni tatizo sugu.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ujangili Hifadhi ya Mikumi, Davis Mushi, anasema ujio wa utalii huo ni faraja tosha kwa vijana waliokuwa hawana ajira katika Mji wa Mikumi, hata hivyo changamoto ya kushindwa kujua lugha za kigeni, imekuwa ni kikwazo kwa baadhi ya vijana, kushindwa kunufaika na fursa hiyo.

“Licha ya fursa hiyo waliyonayo vijana bado changamoto ya kujua lugha ya kigeni ni kikwazo kwa baadhi ya vijana,” anasema Mushi.

Kwa upande mwingine anasema uongozi wa Hifadhi ya Mikumi kupitia kitengo cha ujirani mwema, umeshiriki kikamilifu katika kuunga mkono jitihada zilizoonyeshwa na vijana hawa, katika uanzishwaji wa utalii huo wa kitamaduni, kwani umewasaidia kuwasogeza karibu na wananchi ambao wanaishi pembezoni mwa vijiji vinavyoizunguka hifadhi hiyo.

Wakati vijana wa Mikumi wakija na utalii huo wa kimataduni, Hifadhi ya Mikumi nayo haiko nyuma katika kubuni vivutio vingine vya utalii, ambavyo vitazidi kuifanya iendelee kuwa mojawapo ya hifadhi yenye upekee nchini.

Naye Ofisa Ikolojia Mikumi, Samweli Mhohachi, anasema uongozi wa Hifadhi ya Mikumi umeendelea kutoa kilio kwa Serikali kwa kuiomba iharakishe ujenzi wa kuchepusha Barabara ya Kilosa-Mikumi ili kunusuru vifo vya wanyama wanaogongwa na magari yanayopita hifadhini.

Mhohachi anasema pia utupaji ovyo wa taka unaofanywa na baadhi ya wasafiri wanaopita katika barabara hiyo, nalo ni janga jingine ambalo limeonekana kuathiri mfumo wa ekolojia kwa baadhi ya wanyama, wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Anabainisha kuwa kutokana na wingi wa taka zinazotupwa katika hifadhi hiyo na wasafiri wanaotumia barabara ya Dar es Salaam- Zambia, imeilazimu MINAPA kuingia mkataba na kikundi cha mazingira na maendeleo kwa ajili ya kuokota taka hizo ambazo huwa wastani wa tani moja kwa mwezi, kitendo ambacho kinawaathiri kutokana na kutumia gharama kubwa katika kukabiliana na changamoto hiyo amabayo si ya lazima kama wadau wangekuwa wanajali wanyama.

Hata hivyo, anasema licha ya kukabiliana na changamoto hizo lukuki, lakini bado hifadhi ya Mikumi imeendelea kufanya vizuri katika kupokea watalii kutoka ndani na nje ya nchi, ambao wameendelea kuja na kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hii, yakiwemo makundi ya twiga, swala, impala pamoja na wanyama wengine na hivyo kuliongezea pato taifa bila kuainisha kiasi cha kipato hicho.

Hata hivyo, anatoa wito kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hususani kwa zile za jamii za wafugaji, kuacha tabia ya kuingiza mifugo yao hifadhini, kwani kitendo hicho kimesababisha magonjwa kutoka kwa mifugo hiyo na kuhamia kwa wanyama pori na matokeo yake kuathiri mfumo wa ekolojia kwa wanyama wanaopatikana hifadhini.

“Pia natoa wito kwa wananchi wanaojishughulisha na kilimo katika vijiji kuacha tabia ya kuendesha kilimo pembezoni mwa hifadhi kwani kitendo hicho kinaweza kuzuia njia za asili za wanyama,” anasema.

Nao baadhi ya wananchi wanaoishi jirani kuzunguka hifadhi hiyo akiwamo Salome Saleh na Nasaliani Toroka, ambao pia ni wanufaika wakuu wa mradi huo wanasema imewapelekea kuwa na uhakika wakuuza bidhaa zao kwa watalii wanaokuja kutembelea hifadhi hiyo.

“Pia mradi huu wa utamaduni umetusaidia kuwa na uhakika wa kipato na hata vijana wengi kubadili mtizamo wa kufanya ujangili ili wapate fedha lakini kwa hivi sasa wanafanya shughuli za utamaduni na kupata tija.

Wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Mikumi, ni jukumu lao kuhakikisha wanashirikiana na uongozi wa hifadhi hiyo katika kulinda na kuitunza pamoja na kupiga vita vitendo vya ujangili ambavyo vimeendelea kufanywa na baadhi ya wananchi na kwa upande wa uongozi hifadhini.

Hata hivyo, ni wakati sasa umefika kwa wadau na Serikali kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na hifadhi ya Mikumi za kuwawezesha vijana kuanzisha utalii huo wa kitamaduni, kwani kwa kufanya hivyo kutazidi kuitangaza hifadhi hii na kuongeza idadi ya watalii na kutokomeza kabisa vitendo vya ujangili vinavyofanyika katika baadhi ya mbuga zilizopo nchini.

Ujio wa utalii huo ni faraja tosha kwa vijana waliokuwa hawana ajira katika Mji wa Mikumi – Davis Mushi

Lango kuu la kuingilia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.