Waziri Mhagama ataka maadili yasimamiwe

Mtanzania - - Kanda - Na AMON MTEGA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amewaomba viongozi wa dini na taasisi zake ziendelee kusimamia maadili kwa jamii ili Taifa liendelee kusonga mbele.

Wito huo aliutoa juzi wakati akitoa salamu za Serikali katika Jubilei ya miaka (75) ya Seminari Kuu ya Peramiho ya Mtakatifu Agustino Jimbo Kuu la Songea.

Waziri Mhagama, akitoa salamu hizo kwenye jubilei hiyo ambayo ilihudhuriwa na maaskofu kutoka majimbo mbalimbali ya ndani ya nchi na nje, alisema umefika wakati wa kuendelea kutenda mema.

Alisema maadili yakisimamiwa kikamilifu, Taifa litakuwa na watu wenye hofu ya Mungu na hatimaye jamii nzima itasongambele kimaendeleo.

Alisema tayari imeonyesha njia namna ya kukabiliana na baadhi ya viongozi ambao walikuwa si waadilifu katika kutekeleza majukumu ya jamii.

Alisema kutokana na Serikali kuonyesha njia, ni vema viongozi wa dini na taasisi zake kuendelea kuiunga mkono kwa kusimamia maadili kwa waumini wao ambao wanawaongoza.

Alisema Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na taasisi hizo za kidini katika masuala ya kuzihudumia jamii ndiyo maana imetoa msamaha wa ada ya vibali vya kufanya kazi kwa wamisionari wanaoingia nchini.

Naye Askofu Martin Mtambuka, aliupongeza uongozi wa Rais Dk. John Magufuli kuwa unakwenda kwenye njia stahiki zinazotakiwa kwenye jamii kwa kuiamsha misingi ya kiuongozi iliyoachwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Pia aliwataka wana semina kufanya kazi kwa bidii, zikiwemo za mikono ili kuachana na mawazo ya kuwategemea wafadhili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.