Julio: Siwaelewi Simba

Mtanzania - - Michezo/Matangazo - Na JENNIFER ULLEMBO -DAR ES SALAAM

ALIYEWAHI kuwa kocha mkuu wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema timu hiyo ina wachezaji wazuri lakini anashangazwa kushindwa kuonyesha kiwango bora walipocheza na Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita.

Julio ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya Dodoma FC, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, ikimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa inaongoza katika Kundi C, alisema katika mchezo wa Jumamosi iliyopita, Yanga walionekana kuonyesha kiwango bora tofauti na Simba.

Julio alisema asilimia kubwa ya wadau walitegemea Simba ingeshinda mchezo ule lakini walichokuwa wakikifanya uwanjani hutegemei na uimara wa timu hiyo.

Alisema limekuwa ni jambo la kushangaza kwa mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, wakati Yanga kipindi cha kwanza hawakuonyesha kiwango bora.

“Yanga wamecheza vizuri, ni mabingwa msimu wa tatu sasa mfululizo, kikosi chao ni kil e kile hakina mabadiliko sana ukilinganisha na Simba,” alisema.

“Lakini walionyesha kiwango bora na kizuri ukilinganisha na Simba ambao msimu huu ndiyo timu ambayo imefanya usajili bora kushinda timu zote,” alisema Julio.

Julio alisema mara nyingi makocha wamekuwa wakilaumiwa timu zikifanya vibaya, lakini kupitia mchezo huo kocha Joseph Omog atakiwi kupewa lawama yoyote, kwani ni wazi wachezaji wenyewe walishindwa kuonyesha kiwango kizuri. Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, mabao hayo yalipatikana kipindi cha pili cha mchezo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.