Benki ya karne ya 21 yadai mabadiliko

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Na PATRICK MUSUSA

BENKI ya karne ya 21 ni benki ya mwaka 2017, ni benki ya kisasa inayowafikia wananchi wote popote walipo kwa kutumia mfumo shirikishi wa uwakala pamoja na mfumo bora wa kidijitali wa kutoa huduma kwa njia ya simu ya mkononi au “mobile”.

Benki ya karne ya 21 inashiriki moja kwa moja katika kukuza sekta ya fedha nchini kwa kutoa elimu, kupitia mawakala na matawi yake, kwa wateja pamoja na raia kuhusu matumizi na faida za huduma mbalimbali za kifedha. Benki ya karne ya 21 inatoa bidhaa na huduma zinazotatua changamoto na kukidhi mahitaji ya wateja wa aina mbalimbali na vigezo na masharti ya bidhaa za benki hii ni rahisi kabisa kueleweka na wateja wenye elimu za viwango vyote.

Bidhaa za Benki ya Karne ya 21 haziwezi kulinganishwa na bidhaa za mabenki mengine.

Benki ya karne ya 21 haiuzi akaunti za hundi, akiba, mikopo na kutuma fedha. Bali benki ya karne ya 21 inauza utatuzi wa changamoto mbalimbali za wateja wake pamoja na huduma mbalimbali za kukuza utajiri wa wateja wake na inatoa huduma zote hizi huku ikimuelimisha na kumshirikisha mteja wake katika kila hatua ya matumizi ya fedha zake.

Benki ya karne ya 21 ni matarajio ya kila benki hapa nchini. Na katika kutimiza matarajio haya ya benki ya kisasa mabenki mengi nchini yamezidi kuingia ubia na wadau mbalimbali katika utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na mawakala na vile vile kushirikisha mifumo mipya ya kidijitali katika huduma zake. Hivyo basi, badala ya kukuza biashara kwa kuajiri wafanyakazi wapya mabenki yameelekeza juhudi nyingi zaidi katika teknolojia mpya ili kupunguza uhitaji wa wafanyakazi.

Awamu tatu za mabadiliko

Huduma za kibenki nchini zimepitia awamu tatu za mabadiliko katika miaka 56 ya uhuru.

Mara baada ya uhuru wateja wa benki walikuwa wanalazimika kwenda katika tawi la benki kwa ajili ya kupata huduma za aina zote. Benki ilikuwa haisumbuki sana kupata wateja wala miamala ya kutosha.

Mwaka 1993 Serikali ilipitisha sera mpya ya kiuchumi ambayo iliruhusu mabenki kutoka nje ya nchi kufungua biashara hapa nchini kwa lengo la kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wote.

Hadi mwaka 2007 kulikuwa na mabenki 40 yakitoa huduma nchini. Matawi mapya ya benki yalikuwa yakifunguliwa kila mwaka na fursa za ajira zilikuwa ni nyingi katika sekta ya kibenki.

Mnamo mwaka 2008, huduma ya kutuma pesa kwa njia ya simu za mkononi ilianzishwa hapa nchini.

Ujio wa mfumo huu mpya wa fedha kwa njia ya simu ya mkononi uliwapa wateja uhuru wa kipekee. Hii ilisababisha upungufu wa wateja wa kibenki pamoja na kushuka uwingi wa miamala ya kibenki na ilipelekea mabenki mengi kuanzisha huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi.

Mnamo mwaka 2010 baadhi ya mabenki yalianzisha huduma za uwakala kwa kushirikiana na wafanyabiashara wadogo.

Kwa kuondoa uhitaji kwa benki kupangisha eneo la biashara na kujenga tawi la benki, mfumo wa uwakala au “agency banking” umewezesha mabenki kutoa huduma katika maeneo ya mbali zaidi na kwa gharama ndogo kuliko ujenzi na uendeshaji wa tawi kubwa la benki.

Ukuaji wa sekta ya fedha Tanzania

Finscope ni utafiti wa kitaifa unaolenga kutoa uelewa mpana kuhusu hali ya huduma za kifedha nchini kwa kuangalia pande zote mbili za masoko ya fedha, utolewaji (supply) na uhitaji (demand) wa huduma za kifedha, katika kubaini mahitaji na tabia za watumiaji wa bidhaa za kifedha. Katika mchakato huu utafiti unabaini uhalisia wa huduma za kifedha pamoja na matumizi yake.

Matokeo ya Finscope ya mwaka huu 2017 yameonyesha ukuaji mkubwa katika sekta ya fedha nchini kwa kuashiria kuwa asilimia 65ya Watanzania wanafikiwa na huduma mbalimbali za fedha, tofauti na Finscope ya mwisho ya mwaka 2013 iliyoashiria asilimia 51 tu ya Watanzania kufikiwa na huduma za kifedha.

Matokeo hayo pia yalionyesha kuwa bado chini ya asilimia 30 ya Watanzania wanamiliki au wameshawahi kumiliki akaunti za benki.

Kwa mtazamo mwingine unaweza ukashangaa kwamba kuna benki 60 hadi mwaka huu 2017 lakini wateja wa kibenki wanafikia jumla ya milioni 7 tu. Vile vile kuna makampuni 7 ya simu hapa nchini lakini idadi ya wateja wa “pesa kwa simu” inazidi milioni 30!

Hii ina maana gani kwa mabenki?

Mabenki mengi nchini yamekuwa yakiuza bidhaa zinazofanana. Akaunti ya hundi ni ile ile katika benki zote. Mikopo ya nyumba ya mabenki mbalimbali yanatofautishwa tu kwa kiwango cha riba. Kinachosahaulika na mabenki ni kwamba, wateja hawafanani. Kila mmoja anapitia changamoto za aina tofauti katika kutimiza malengo yake ya maisha.

Ili kuwa kinara kati ya mabenki 60 nchini benki inapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:

Kwanza, lijue soko lako au wajue wateja wako.

Pili, lenga kuwa benki bora inayohudumia wateja wa aina hiyo.

Tatu, katika kutanganza bidhaa za kibenki, jitihada ziwekwe katika kutofautisha faida za bidhaa za benki yako na za benki nyingine. Vyema zaidi mteja akipata huduma au “experience” ya kipekee anapokuja kwenye benki yako kwa ajili ya kununua bidhaa au kupata huduma maalumu.

Je, kwa mabenka? Na wanaotafuta ajira katika sekta ya kibenki?

Hivi karibuni mabenki mengi yamebadilisha mikakati ya kibiashara na kuelekeza juhudi kwenye mifumo ya kidijitali na ya uwakala. Hii imepelekea kupunguzwa kwa idara mbalimbali ndani ya mabenki hayo na hivyo kuweka mashakani ajira za wafanyakazi wengi.

Lakini si wafanyakazi wote huishia kupunguzwa kazi kwa sababu ya utaratibu mpya bali wafanyakazi wanaopokea mabadiliko kwa mtazamo chanya na kutafuta nafasi zao katika ulimwengu mpya wa kazi huweza kustahimili vipindi hivi vya “retrenchment”.

Hivyo basi katika benki ya karne ya 21 wafanyakazi hujishughulisha kujifunza vitu vipya na kuboresha ufanisi wao. Vyema zaidi, wafanyakazi hawa wanatambua umuhimu wa vipaji vidogo au “soft skills” katika utendaji wao.

Karne ijayo

Ikiwa kwamba mabadiliko ya awali katika sekta ya kibenki yaliletwa na mabenki yenyewe, mabadiliko ya karne hii yamekuwa yakichochewa na wateja wenyewe. Siku hizi wateja wana uhuru wa kuchagua mabenki ya kuwahudumia na wasipopenda huduma huweza kuhama mara moja. Vyema zaidi, wateja wa karne hii wanafikiwa na taarifa za aina nyingi na kwa haraka zaidi na hivyo mahitaji yao yamekuwa ya aina nyingi na ya haraka zaidi.

Katika karne ya mabadiliko ya mwendo kasi, mabenki pamoja na wafanyakazi wake wanapaswa kutambua kuwa usalama wao katika biashara na ajira unaenda sambamba na uwezo wao wa kujiendeleza na kubuni mbinu mpya za kufikisha huduma kwenye soko kubwa zaidi kila siku.

(Patrick Mususa ni Mkurugenzi Mtendaji, Tainzania Institute of Bankers (TIOB).

Ujio wa mfumo mpya wa fedha kwa njia ya simu ya mkononi uliwapa wateja uhuru wa kipekee. – Patrick Mususa

Matumizi ya teknolojia ya digitali kutamaki shughuli za benki karne 21

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.