Uwiano kijinsia katika huduma za fedha wahitajika

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - shermarxn@gmail .com

TAKWIMU zote za kiuchumi na kisera zinaonesha kuwa kuna pengo kubwa la maendeleo na kipato kati ya jinsia na huku ikithibitika kuwa wanawake wengi bado wako nyuma kiuchumi ukifananisha na hali ya wanaume. Hayo ni matokeo ya historia ambayo kwa miaka mingi sana wanawake wamebanwa na mifumo dume ambayo ilikuwa inampendelea mwanamume na kumnyanga’anya mwanamke ingawa idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume kutokana na matokeo ya takwimu mbalimbali.

Matahalani kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote ni wanawake, hivyo kutokana na takwimu hizo Serikali haina budi kuhakikisha inawawekea mazingira mazuri na wezeshi ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Kwani kuwainua wao ni sawa na kunusuru nusu ya watu wa Taifa hili.

Pamoja na wingi wa wanawake kutokana na uduni uliochagizwa kwao, wamekuwa wakijihusisha na biashara ndogondogo ambazo hazina uwezo wa kuwatoa katika lindi la umasikini na hivyo tatizo kudai ushiriki wa wadau wengi.

Utafiti uliofanywa na kituo cha sera za biashara Afrika (ATPC), umebainisha kuwa biashara inatoa ajira kwa asilimia 60 ya wanawake kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania na asilimia 70 hadi 80 yao wamejikita katika biashara isiyo rasmi na hivyo kuendeleza uduni wa maisha na kudai mabadiliko.

Mfumo dume uliokuwepo umewafanya wanawake wawe duni katika mambo mbalimbali na hasa yale yahusuyo uchumi na maendeleo.

Takwimu zilizotolewa na Shirikia la UN Women zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 74 ya wafanyabiashara za mipakani katika nchi za maziwa makuu ni wanawake na wengi huishia kubangaiza tu bila mafanikio makubwa.

NMB yaingilia hali

Benki kubwa kuliko zote kwa mali na hali nchini, Benki ya NMB imeliona tatizo hilo na katika mkutano wa Women’s World Banking kuwa inalifanyia kazi vilivyo suala hilo kwa umakini wa kuleta uwiano wa kijinsia katika huduma zake.

Mkuu wa Idara ya Fedha za Kigeni katika Benki ya NMB, Gladness Deogratias, amesema katika mdahalo kuhusu uwiano wa kijinsia katika mkutano wa Women’s World Banking, ambao unalenga kuangalia namna bora ya kuwafikia wanawake katika maeneo mbalimbali duniani ili wapate huduma za kifedha katika upeo mpana wa Azimio la Maya.

Gladness alisema benki hiyo inatambua umuhimu wa kuwa na uwiano wa kijinsia wa wanaume na wanawake kuanzia kwa wafanyakazi wake mpaka aina ya huduma ambazo wanazitoa kwa wateja wake.

Alisema NMB imekuwa na sera bora ambazo zinawapa nafasi sawa wanawake na wanaume katika vyeo mbalimbali vya ofisi, kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo namna wanavyoweza kufanya kufanikiwa na wajasiriamali kutoa mafunzo kuhusu njia bora ambayo wanaweza kuitumia kuendeleza biashara zao.

“Uwiano wa kijinsia katika mashirika ni muhimu ili kuwapa nafasi wanawake washiriki katika shughuli za maendeleo, kwetu NMB wanawake wanapewa nafasi hii inatokana na benki yetu kuwa na sera bora zinazozingatia uwiano wa wafanyakazi wake kuanzia wafanyakazi wetu wa kawaida hadi viongozi, lakini pia tuna Jukwaa la Wanawake ambalo linatumika kutuunganisha,” alisema na kuongeza kuwa changamoto kubwa ambayo inawapata wajasiriamali wanawake ni kutokuwa na elimu ya hesabu ya kutunza taarifa zao za kuuza na kununua bidhaa ili wanapokwenda benki wapatiwe mikopo kwa urahisi.

Jambo hilo linashughulikiwa kikamilifu na mpango wa Business Club wa NMB ambao unatoa mafunzo kwa wajasiriamali ikiwamo wale wanawake.

Kwa wajasiriamali wanawake, Benki ya NMB ina akaunti ya pamoja ambayo inatumiwa na vikundi na hivyo kuwataka wanawake kuitumia akaunti hiyo kwani ina huduma za kisasa ambazo zinaweza kuwasaidia kukuza biashara zao na kuinuka kiuchumi.

Ukweli ni kuwa Akaunti ya Pamoja ina huduma ambazo hazipo katika akaunti za kawaida na hivyo wanawake wataweza kuona hesabu zao vizuri na imeboreshwa kwa kupata huduma kwenye simu. Akaunti hiyo imeendelezwa na inakuwa si kama zamani ambapo ilikuwa ukitaka kuchukua mkopo mpaka mweka hazina awepo, lakini kwa sasa wateja wanaweza kutumia NMB Mobile Banking.

Hali hiyo inaufanya Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia (GTI) na ya mafunzo ya kushirikishana jinsi ya kuingiza au kuhakikisha masuala ya jinsia yanaingizwa katika michakato ya biashara.

Benki ya NMB Tanzania imesema mbali na kutoa huduma bora kwa wateja wake, itazingatia uwiano wa kijinsia kwa kuwapa wanawake na wanaume nafasi sawa za kushiriki shughuli za maendeleo.

Isitoshe mafunzo hutolewa katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), CBE na UDSM ambapo wanawake hupewa mbinu ambazo wanaweza kuzitumia kupata nafasi ya kufanya kazi benki.

Vilevile Jukwaa la wanawake la NMB linafanya kazi kwa karibu na kitengo cha Business Bank kwa kutoa mafunzo kwa Klabu za Biashara (Business Club) na kuweka mbele dhana ya kuwa ukiweza kumkomboa mwanamke kiuchumi umekomboa jamii nzima.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.