Tamu, chungu biashara maduka makubwanchini

Mtanzania - - Biashara Na Uchumi - Inatoka uk i

Wiki mbili zilizopita maduka makubwa mawili ya Nakumatt katika Tawi la Dar es Salaam na Arusha yalifungwa kwa kile kinachadaiwa kushindwa kulipa kodi ya jengo.

Kuyumba kibiashara kwa Nakumatt yenye makao yake Nairobi Kenya, kulianza nchini humo kwa kufunga matawi yake kwa sababu ya kujiendesha kwa hasara. Tunauliza kulikoni? Kwani wachuuzi wa bidhaa kwa maduka haya inaonekana wameachwa solemba katikati ya barabara na hivyo kukwama na huku hakuna njia ya kutokea kwani akilini bado yaliyowakuta kwa maduka ya uchumi bado suluhisho halijapatikana. Isitoshe hakuna mamlaka iliyokuja mbele kutoa maelezo ya hali iliyofikiwa na kutia shaka huenda wakubwa wamo humu ndio maana mambo yanakwenda kombo na hakuna linalofanyika.

Historia ya maduka makubwa

Miaka michache iliyopita maduka makubwa ya kimataifa yalifunga biashara zake kama Shoprite na Uchumi kutokana kujiendesha kwa hasara na sasa Nakumatt imeingia katika hali tete katika maduka yake yote yaliyopo nchini na hivyo kuleta taharuki.

Historia inaonesha tangu mwishoni mwa miaka ya 90 biashara ya maduka ya kisasa ambayo yanaendeshwa na wawekezaji wa nje yalianza kuingia nchini, lakini hayadumu katika biashara hiyo kutokana wanachodai kuzalisha faida ya kiwango cha chini hivyo kulazimika kufunga biashara au kuuza kwa makampuni mengine.

Mwaka 2000 maduka ya Score kutoka Afrika Kusini yalifunguliwa na baadaye yakafunga biashara na kuiuzia Shoprite baada ya miaka kadhaa Shoprite nayo ikauzwa kwa Nakumatt. Miaka miwili iliyopita, Uchumi kutoka nchini Kenya ilifunga shughuli zake nchini kutokana na kujiendesha kwa hasara.

Kwa sasa maduka makubwa ambayo yanaendelea na biashara nchini ni pamoja na Game kutoka Afrika Kusini na Choppies ya Botswana ambayo yote yapo Dar es Salaam. Kwanini biashara inakuwa ngumu hivyo?

Anguko la Nakumatt

Wiki moja kabla Nakumatt kufungwa Mlimani City, MTANZANIA ilitembelea duka hilo na kukuta upungufu wa bidhaa kwa kiasi kikubwa sana katika sehemu za kuhifadhia bidhaa zikiwa wazi (rafu za wazi bila bidhaa), kitu ambacho si cha kawaida kwa duka kubwa kama hilo.

Vilevile katika duka la Nakumatt Arusha kabla halijafunga, gazeti hili lilifuatilia katika tawi hilo na kukuta duka hilo kuishiwa bidhaa katika rafu zake. Vitu ambavyo vilionekana ni nguo na vitu vichache na wafanyakazi wa duka hilo wamebakia wamejiinamia.

Hata hivyo, hali halisi ya biashara katika maduka yake nchini Kenya inaendelea kudorora baada ya kufunga baadhi ya maduka yake nchini humo.

Sababu za kunywea huko ni nyingi na hakuna uwazi wa kujua mengi. Nakumatt yenye maduka makubwa Afrika Mashariki yote inadaiwa kuwa ina usimamizi mbaya, mipango ya upanuzi mibovu na ikiwemo ongezeko la ushindani kwenye soko hasa nchini Kenya ni mojawapo ya sababu ya kudorora kwa maduka hayo. Nchini suala la umahiri wa ‘duka la Mchaga’ nao ni tatizo kwao.

Kwa mujibu wa Andrew Dixon, Mkuu wa Masoko wa Nakumatt, Julai Shirika la Habari la Telegraph lilimnukuu akisema hali ya biashara nchini Kenya imekumbwa na dhoruba ambapo mfululizo wa matukio yamekusanyika ili kujenga nafasi ya Nakumatt kuporomoka.

Nakumatt imeshindwa kuwalipa wasambazaji ambao kwa sasa huhitaji kulipwa kabla ya kuleta bidhaa au mkono kwa mkono na huku wamiliki wa majengo wakishikilia bidhaa ili kufidia madeni ya awali ya kodi.

Aidha, Dixon aliongeza kuwa moja ya mambo yaliyochangia Nakumat kuanguka ni shambulio la kigaidi la Westgate lililotokea Septemba 2013, jijini Nairobi, Kenya.

Pia sekta ya maduka makubwa ya rejareja nchini humo imeshuka maradufu kutoka asilimia 12 hadi asilimia 6.

“Tulikuwa tumeunganisha mpango wa biashara ambao ulikuwa na ukuaji fulani katika uchumi. Ukuaji huo umepungua,” alisema Dixon.

Mapema Julai mwaka huu, duka la Nakumatt Nairobi lilifungwa kutokana na kudaiwa kodi na mmiliki wa jengo ambaye alilazimika kuhodhi baadhi ya mali za Nakumat ikiwamo magari (malori), runinga, friji kwa lengo la kuyapiga mnada ili apate Shilingi za Kenya milioni 51.

Hadi kufikia sasa maduka ya Nakumatt nchini Kenya yanaendelea kufungwa na hakuna dalili za kufanikiwa baada ya Serikali na wadau kukataa kuongeza mtaji.

Malimbikizo ya madeni

Biashara ya Nakumatt ilianguka rasmi pale duka lake la Mlimani City jijini Dar es Salaam kufungwa baada kudaiwa kodi ya Sh milioni 300 ya miezi mitatu. Pia Tawi la Arusha lilifungwa kwa madai ya madeni kama hayo kwa wamiliki wa majengo.

Meneja Mkuu wa Mlimani City, Pastory

Mrosso, anasema sababu za kufungwa huko ni kutokana na kudaiwa kodi ya miezi mitatu mfululizo. Aidha, sababu nyingine ni kupungua kwa ufanisi mpaka chini ya wastani.

“Bidhaa wanazostahili kuwa nazo hazikidhi mahitaji. Zimepungua kuliko viwango vinavyokubalika,” anasema Mrosso.

Wiki iliyopita mamia ya wasambazaji wa bidhaa ambao wanadai Nakumatt mabilioni ya shilingi, walisema kwamba mfanyabaishara Yusuf Manji yupo kwenye mazungumzo kununua maduka hayo nchini.

Msemaji wa wasambazaji hao, Joseph Mlay, aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano, kwamba wanaamini mazungumzo hayo yataenda vizuri ili waweze kulipwa kiasi madeni yao.

Kwa upande wa Tanzania, Mfanyabiashara ambaye ametaka jina lake lisitajwe, aliliambia MTANZANIA kuwa amekuwa akisambaza bidhaa katika maduka makubwa kwa kipindi kirefu ambapo changamoto kubwa ni kukopwa na kucheleweshewa malipo.

“Maduka haya wanasumbua kulipa madeni, inahitaji juhudi kubwa kufuatilia au ukiwatisha kuwa unaenda kwenye vyombo vya sheria, hapo angalau malipo yako yanaweza kulipwa,” alisema. Inaonekana kuwa mengi ni kijungu jiko tu.

Vyombo vya habari nchini Kenya viliripoti kufikia Aprili mwaka huu, Nakumatt ilikuwa na madeni yanayokadiriwa kufikia Ksh bilioni 18 kutoka Ksh bilioni 4.7 mwaka 2012.

Mwezi Oktoba mwaka jana, wasambazaji wa bidhaa nchini Uganda walisitisha kupeleka bidhaa katika duka hilo kutokana na kushindwa kulipa madeni, hivyo kusababisha kufungwa kwa maduka ya nchini Uganda.

Hali ya biashara nchini

Baadhi ya mambo yanayochangia kutokwenda kwa kasi kwa maduka hayo ni uzalishaji wa faida ndogo ukichangia na utamaduni wa Watanzania kuhusu manunuzi, ambapo wengi hununua bidhaa katika maduka mitaani yaliyopo karibu na makazi yanayojulikana kama kiosk cha Mchagga.

Maduka makubwa hufanya vizuri katika nchi ambazo uchumi wake ni mkubwa kama Afrika Kusini, ambapo watu hutegemea manunuzi ya madukani kwa kadi za mkopo wa mashirika au mabenki.

Katika upande wa Soko la Kenya, kwenye biashara ya maduka ya kisasa inafikia thamani za Dola za Marekani bilioni 23.7 takwimu ya mwaka 2013 kwa mujibu wa ripoti ya Deloitte ya African Powers of Retailing New Horizons for Growth iliyotolewa 2016. Ripoti ya Deloitte inasema kwa upande wa Tanzania inayo mazingira ya kuvutia kutokana kuwa katika Pwani ya Bahari ya Hindi.

Pia maduka hayo humilikiwa na wawekezaji wa nje na bidhaa nyingi huagizwa kutoka nje. Kitu kingine ambacho kinachangia ni kupatikana nje ya miji ambapo huhitaji gharama za usafiri huku maduka hayo kufunguliwa kwa muda maalumu ambapo wanunuzi wengi wako kazini.

Francis Ngaweje ni mkazi wa Manzese ambaye hufanya shughuli zake maeneo ya Mwenge, anasema kuwa bidhaa za maduka ya kisasa bei yake ni ghali.

“Siwezi kununua robo kilo ya sukari supermarket, kwa sababu nitahitaji nauli, nadhani maduka hayo ni kwa ajili ya watu wenye pesa nyingi na si kwa watu wa kipato cha chini kama mimi,” alisema.

Biashara miaka mitano ijayo

Kwa mijibu wa Ripoti ya The Grocery Retail Market Tanzania iliyotolewa na Kampuni ya utafiti wa biashara ya Businesswire kuhusiana na masoko ya maduka ya kisasa, inaangalia hali halisi ya sekta hii nchini katika miaka mitano ijayo.

Ripoti hiyo inasema kuwa kiwango cha ukuaji wa miji nchini kitaongezeka mara mbili kutoka asilimia 28.6 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 50 mwaka 2050 yaani 50 kwa 50.

Hivyo idadi ya wateja wa maduka makubwa itaongezeka mara mbili zaidi kutoka milioni 15 mwaka 2015 hadi kufikia milioni 64.6 ifikapo 2050 hasa Dar es Salaam na ongezeko hilo inasemekana litatoka kwa watumiaji wa hali ya chini. Wanyonge siki zote ndio soko la kubadili msimamo kutokana na wingi wao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inachukuliwa kuwa katika nchi 10 bora kwenye biashara ya maduka ya kisasa zaidi ya Afrika kutokana na wingi wa watu wake na ukuaji wa uchumi wenye uhakika.

Soko la Tanzania mara nyingi huonekana ni dogo ikilinganishwa na Kenya, lakini inabainisha kuwa Tanzania inatoa mazingira ya wazi kwa wawekezaji wa nje kwa sababu ya ukosefu wa maduka hayo.

Kwa sasa, Shoppers, Shrijee na Nakumatt wanashikilia kwa usawa soko la Dar es Salaam kwa watu wa kipato cha kati na bidhaa nyingi zinaagizwa kutoka Kenya, Dubai, India na Ulaya. Watakapokuja Wachina hali ya soko itabadilika sana hasa baada ya East Africa Logistics Centre kujengwa na kuanzisha shughuli zake pale Ubungo ambapo kutakuwa na maduka makubwa, maghala na viwanda vidogo sehemu kama 3,000 za biashara kukiwa na lengo la kuzuia wafanyabiashara kwenda China na kupata bidhaa zao nchini na kuifanya Dar es Salaam ifanane na Dubai.

Linghang Group

Dar es Salaam itapata shughuli kubwa ya uwekezaji katika Wilaya ya Ubungo, ambapo zaidi ya nafasi 3,000 za biashara zitaanzishwa kwa kile kinachoitwa awamu ya kwanza ya East African Commercial and Logistics Centre (EACLC) na kujengwa kwenye eneo ambalo sasa ni kituo kikubwa cha mabasi Ubungo Bus Terminal (UBT).

Kampuni hiyo kutoka China ni mwendelezo wa wazo kama hilo kuhusu Tanzania Logistics Centre la kuendeleza Kurasini na Bandari na sasa limeibuka huko Ubungo na kutegemewa kujengwa kuanzia Novemba 6, ambapo litawekwa jiwe la msingi.

Kampuni ya Linghang Group kutoka Shanghai China ndio mwekezaji mkuu ambaye Mwenyekiti wake wa Bodi, Lisa Wang, anasema uwekezaji huo utafanyika baada ya kupata hati ya umiliki ya eneo hilo katika Wilaya ya Ubungo na itakuwa mojawapo ya nguzo za uchumi wa wilaya hiyo.

Lisa alisema wanafurahi kumaliza vihunzi vyote vya uwekezaji na wanategemea sasa kuanza kujenga eneo hilo la biashara ambalo litakuwa kubwa sana lenye eneo la mita za mraba 124,000 katika awamu ya kwanza na kuwa na maduka 3,000 na maghala 300 nafasi za kuegesha magari 5,000 na kujenga miliki za makazi na sehemu za mabenki, kodi, huduma za mizigo na usafiri, usimamizi na usalama na vile vinavyohusikana navyo.

Anasema EACLC itaajiri zaidi ya watu 20,000 wakiwa ni wenyeji na itahusu biashara ya thamani ya dola bilioni 44 ifikapo 2019 na kukisiwa kuongezeka kila mwaka kwa kiasi cha asilimia 30 na hivyo kitegemewa kuwa kigezo kizuri na kikubwa kwa maendeleo ya nchi na biashara ya Afrika ya Mashariki.

Linghang Group mpaka sasa inaundwa na Linghang Food(Shandong) Co ltd, Linghang Food (GuangDong) Co; Ltd, Lisa & Mike International, Linghang Tanzania Corporation na Golden Dragon (HK) Ship Corporation.

Maduka makubwa yenye ushindani nchini ni pamoja na Fruit and Veg City, Imalaseko, Massmart, Nakumatt, Shoppers, Shrijee’s, TSN na Village.

Tuskys, Nakumatt wataka kuungana

Habari toka Nairobi zinasema mitandao hiyo ya maduka imeiandikia Mamlaka ya Ushindani ya Kenya (Competition Authority of Kenya -CAK) nia yao ya kutaka kuungana.

Tuskys Supermarkets imeeleza nia yake ya kuungana na mshindani wake mkubwa Nakumatt ili kukwepa kampuni hiyo yenye matatizo ya kipesa isifilisiwe.

Mtendaji Mkuu waTuskys, Dan Githua kwa pamoja wameandika barua kwa CAK ikiwajulisha nia yao na kutaka baraka za kutozuiwa na kutafuta msimamo wake kuhusu hoja hiyo.

Nakumatt inatishiwa maisha katika miezi ya karibuni baada ya kukosa mtaji mpya na kushindwa kupata ahueni na kudaiwa kutoka kila upande wa mahusiano yake ikiwamo mishahara ya wafanyakazi, wachuuzi mali na wakopeshaji. Inafikiriwa kuungana na Tuskys kwani mategemeo ya kuokolewa na Serikali kwa mkopo zimegonga mwamba.

Mkurugenzi Mkuu wa CAK, Wang’ombe Kariuki, amethibitisha hali hiyo na anasema mawasiliano yake na wahusika yamefanyika tayari bila kusema mengi.

Kama itafanyika itatengeneza mtandao mkubwa wa maduka nchini Kenya na kuyaacha mbali maduka shindani ya Naivas Supermarket na Uchumi Supermarkets.

Kariuki alisema kama wanataka Mkataba wa Uongozi watahitaji kibali cha ku samehewa (exemption) na kama wanataka kuungana wanatakiwa kufuata sheria na alikubaliana na hali ngumu iliyopo kwenye biashara sekta ya rejareja na kuahidi kushughulikia maombi hayo mara moja yatakapoletwa vyovyote vile.

Mwonekano wa ndani wa duka la Nakumatt lililopo jijini Arusha ilikiwa rafu hazina bidhaa.

Duka la Nakumatt lililopo jijini Arusha lilipoanzishwa lilisheheni bidhaa kila aina.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.