Benki ya Mwalimu yatanua wigo kupitia TPB Plc

Mtanzania - - Biashara - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

BENKI ya Mwalimu Commecial, imetanua wigo wake kupitia mkakati wake na Benki ya Posta (TPB Plc).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mwalimu Commercial Bank, Ronald Manongi, alisema benki yake imeamua kuingia kwenye makubaliano ya kimkakati na benki ya TPB ili kuwawezesha wateja wake kukuza biashara zao kupitia wigo mpana zaidi uliojengwa kupitia makubaliano hayo.

“Benki yetu ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa tunasogeza huduma zetu karibu zaidi na wananchi popote pale walipo. Nia ni kuhakikisha kuwa Mtanzania popote alipo aweze kupata huduma za kibenki ili kwa pamoja tuweze kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema.

Alisema benki hizo zimehakikisha miamala yote ya wateja wao kutoka benki moja kwenda nyingine inafanyika katika hali ya usalama zaidi kupitia mtandao na hivyo kuondoa uwezekano mkubwa wa kufanyika makosa ya aina yoyote. Alisema zimeshirikiana kutengeneza mfumo wa kielektroniki unaoziunganisha utakaowawezesha wateja wa MCB kupata huduma za kibenki kupitia matawi yote ya TPB nchi nzima. Benki hizo zimechukua tahadhari stahiki ili kuhakikisha kuwa mfumo huo unawawezesha wateja wao kupata huduma hizo kwa usalama na haraka.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi, alisema ushirikiano huo una tija kubwa na utawanufaisha wateja wa Benki ya TPB.

“Baadhi ya wateja wa Benki ya TPB wanafanya biashara na wateja wa Benki ya MCB, hivyo ushirikiano huu utarahisisha sana biashara kati wa wateja wetu,” alisema Moshingi.

Alisema ushirikiano huo unalenga kukuza na kuboresha uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na utawawezesha wateja wa Benki ya MCB kupata huduma kupitia mtandao mkubwa wa TPB ulioenea nchi nzima.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.