Shahidi kesi ya Malkia wa Tembo augua

Mtanzania - - Habari - Na KULWA MZEE -DAR EA SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imekwama kuendelea kusikiliza ushahidi katika kesi inayomkabili raia wa China anayedaiwa kuwa Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66) na wenzake wawili kwa sababu shahidi anaumwa.

Mahakama ilikwama jana baada ya Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, kudai shahidi waliyemtarajia mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, bado anaumwa afya yake si nzuri.

Wankyo alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini kutokana na mazingira yaliyopo akaomba kesi iahirishwe.

Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko, hakuwa na pingamizi kwa hoja ya upande wa mashtaka kuomba ahirisho.

Hakimu Shaidi alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, 2017 na kuamuru siku hiyo upande wa mashtaka upeleke mashahidi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase, ambapo wanadaiwa kuwa kati ya Januari mosi, 2000 na Mei 22, 2014 walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali.

Katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889, zenye thamani ya Sh bilioni 13 bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Wanadaiwa kuwa kati ya Januari mosi, 2000 na Mei 22, 2014, kwa makusudi raia wa China, Yang Feng Glan, aliongoza na kufadhili vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo 706 vya meno ya tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Kwa upande wa washtakiwa, Salvius na Manase, wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za Serikali kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza meno ya tembo kwa nia ya kujipatia faida.

Inadaiwa kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari wa Jeshi la Polisi D 7847 Koplo Beatus, ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa ya kujihusisha na biashara za nyara za Serikali.

PICHA: MPIGA PICHA WETU

HUDUMA: Mkurugenzi wa Bidhaa na huduma za Tigo, David Umoh,akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakati wa kuhusu uzinduzi wa kampeni ya ‘Tumekusoma’ ambayo ni mkakati wa kufikia wateja wake nchi nzima.Kulia ni Mtaalamu wa huduma kwa wateja katika kitengo cha Biashara wa kampuni hiyo, Sarah Cyprian.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.