TPA yatenga milioni 75/- kusaidia afya, maji

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU -MWANZA

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imetenga jumla ya Sh milioni 75 ili kusaidia huduma bora za maji safi, afya na elimu kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa moja ya visima vitatu vilivyotolewa na TPA kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, alisema misaada hiyo ni sehemu ya majukumu ya TPA kusaidia jamii inayozunguka.

“Tuna jumla ya bandari 90 nchi nzima na hizo zote inabidi zinufaike kutokana na misaada hii, na ndio maana unaona tunatoa kidogo kidogo kwa majirani zetu kama tulivyofanya leo hapa.

“Alisema kwa Ziwa Victoria pekee, tuna jumla ya bandari 30 wakati katika bandari nyingine kama vile Ziwa Tanganyika tuna jumla ya bandari 25 na Ziwa Nyasa zipo 15, huku zinazobaki zipo katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

“Kwa Kanda ya Ziwa peke yake tumetoa mashuka ya wagonjwa kwenye hospitali za mikoa, vituo vya afya na zahanati na kwa upande wa elimu, tumetoa madawati kwenye shule za msingi mbalimbali pamoja na kujenga visima vya maji safi,” alisema Kakoko.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mwantumu Dau, aliishukuru TPA kwa msaada huo kwani umechangia kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Alisema kwamba hali ya upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo imeongezeka kutoka asilimia 62.4 kwa mwezi Julai, 2016 hadi kufikia asilimia 65.4 kwa mwezi Oktoba, 2017. “Ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa miradi mipya ya maji iliyokamilika katika vijiji 10 pamoja na mradi huu wa visima vitatu tunaokabidhiwa leo,” alisema. Alisema ili kutunza vyanzo vya maji, wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kwa wananchi jinsi ya kutunza vyanzo hivyo pamoja na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira. Kwa upande wa elimu na afya, Mhandisi Kakoko alisema kwamba, TPA imejikita zaidi kusaidia elimu na huduma za afya kwa sababu ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote lile duniani.

“Unapozungumzia maendeleo ya nchi, elimu ndio ya kwanza kabisa kwa sababu hapo ndipo watapatikana wabunifu wa mipango ya maendeleo,” alisema.

Ametolea mfano mataifa kama ya China, Vietnam, Malaysia yamepiga hatua zaidi kimaendeleo ndani ya kipindi kifupi kuliko Tanzania, sababu ya kuwa na watu wenye afya njema na walioelimika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.