Miti hatarishi kung’olewa Mbeya

Mtanzania - - Habari - Na CHRISTPHER NYENYEMBE -MBEYA

WAKAZI wa maeneo ya Ilomba na Iyunga, jijini Mbeya, wameelezea wasiwasi juu ya uwepo wa miti mirefu aina ya mikalatusi (Cyprus), iliyopandwa ama kujiotea yenyewe kandokando ya Barabara Kuu ya UyoleTunduma, yenye umri mkubwa kati ya miaka 30 kwani inahatarisha usalama wa watu na mali zao.

Kwamba miti iliyoota kandokando ya barabara hiyo imekuwa ikitishia usalama wa abiria na magari yanayopita katika maeneo hayo, kutokana na upepo mkali unaovuma kipindi hiki kiasi cha kuwajengea hofu ambapo ameziomba mamlaka zinazohusika kuiondoa miti hiyo.

Mkazi wa maeneo ya Sae, Benard Mwanganya, alisema hakika hiyo miti ni hatarishi kwa maisha ya watu, waenda kwa miguu, abiria waliopo kwenye vyombo vya usafiri na magari mengine yanayosafirisha bidhaa endapo itatokea miti kama hiyo ikaangukia barabarani.

“Angalia miti kama hii eneo la Nane nane upande wa Chuo cha Uyole, ilikatwa lakini bado mingine ipo mita chache kutoka barabara kuu, hii ni hatari kwa kuwa mingine ina umri mkubwa tangu ilipoota ni rahisi kuangushwa na upepo, hasa hii njiapanda ya kwenda Ituha nako ni shida, upepo unatishia usalama wa watu,” alisema Mwanganya.

Diwani wa Kata ya Ilomba, jijini Mbeya, Dickson Mwakilasa (Chadema), alisema malalamiko kuhusu miti analijua na tayari amejipanga kulifikisha katika kikao cha maendeleo cha kata (WDC).

Akizungumzia hali hiyo, Mhandisi wa Matengenezo wa wakala wa Barabara Mkoa wa Mbeya (Tanroad), Given Njiro, alisema mwenye mamlaka ya kuzungumzia uondoshwaji au kulisemea jambo hilo ni Meneja wa Tanroad mkoa na si yeye.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.