Benki ya kilimo kuleta mageuzi Njombe

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU -NJOMBE

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB), imesema imejipanga katika kusaidia kuchagiza kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa wakulima mkoani Njombe.

Ahadi imetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Rehema Twalib, wakati alipouongoza ujumbe wa benki walipomtembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka.

Alisema kuwa TADB ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, ili kuisaidia Serikali kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya nchi.

Aliongeza kuwa Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ili kusaidia kukabiliana na mapungufu hayo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika kilimo nchini.

“Katika kuhakikisha tunafikia malengo ya Serikali, benki imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini, kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” alisema Twalib. Awali akizungumza na ugeni huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, alisema ujio wa benki hiyo mkoani kwake utahamasisha shughuli za kilimo mkoani humo, hali itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Naishukuru Serikali kwa kuianzisha TADB, kwani hali ya ukosefu wa mitaji ya uhakika inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa na kuwasahau wakulima na wasindikaji wa mazao, hivyo tunaamini TADB itasaidia kutatua changamoto hii,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini ya Mikopo wa TADB, Dickson Pangamawe, alisema TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi, wa kati pamoja na ile ya muda mrefu ambayo hulipwa kwa zaidi ya miaka 15. Kwa mujibu wa Pangamawe, mikopo hiyo ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara, ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.