Kiwango kidogo cha uzazi Ulaya chamkera Papa

Mtanzania - - Kimataifa - VATICAN CITY, VATICAN

PAPA Francis amekosoa kiwango kidogo cha uzazi barani Ulaya na kutaka vijana wadogo wasaidiwe wajiandae kwa njia nzuri za wakati ujao katika jamii.

“Ulaya ambayo inajibaini yenyewe kama jamii, ni chanzo cha maendeleo yake na dunia nzima,” Papa aliuambia mkutano wa ‘(Re) Thinking Europe’, mradi unaofadhiliwa na Baraza la Maaskofu wa Katoliki Ulaya (COMECE).

“Ulaya, inaugua kwa kipindi kibaya cha ‘utasa’. Si tu kwa sababu Ulaya ina watoto wachache na wengi kunyimwa haki za kuzaliwa, bali pia kwa sababu kuna kushindwa kutengeneza utamaduni mzuri wanaohitaji vijana kukabiliana na wakati ujao.”

Hii si mara ya kwanza Papa huyo raia wa Argentina kuonyesha kukerwa na kiwango kidogo cha uzazi barani humo kwani mwaka 2014, wakati akilihutubia Bunge la Ulaya aliueleza Umoja wa Ulaya kama ‘bibi mchovu’, ambaye hana uwezo tena wa kuzaa.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya, Frans Timmermans na Mtendaji Mkuu wa Bunge la Ulaya, Antonio Tajani.

Walimsikia Papa Francis akisisitiza Ulaya si chombo cha takwimu au taasisi, bali kilichoundwa na watu, ambao hawapaswi kupukutishwa.

Aidha alisisitiza kuwa viongozi wa Ulaya wana wajibu wa kuhamasisha Ulaya iliyo na jamii jumuishi, badala ya ile ya uwiano mbaya baina ya walio nacho na wasio nacho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.