Waziri matatani kwa kashfa ya ngono Uingereza

Mtanzania - - Kimataifa - LONDON, UINGEREZA

WAZIRI wa Uwekezaji wa Serikali ya Uingereza, Mark Garnier, anachunguzwa kwa tuhuma za kumtaka katibu wake muhtasi kumnunulia midoli ya ngono na kumwelezea kwa lugha mbaya.

Waziri wa Afya, Jeremy Hunt alisema juzi kuwa Ofisi ya Baraza la Mawaziri inayohusiana na ufanisi serikalini, itachunguza iwapo tabia ya Garnier ilikiuka kanuni za maadili za mawaziri.

“Taarifa hizi, iwapo ni za kweli hazikubaliki kabisa,” Hunt alikiambia kipindi cha siasa cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Msemaji wa wizara hiyo, alithibitisha uchunguzi dhidi ya Garnier, baba mwenye mke na watoto watatu, lakini aligoma kufafanua zaidi.

Katibu muhtasi wa zamani wa Garnier, Caroline Edmondson, aliliambia Gazeti la Jumapili la The Mail la hapa kuwa mbunge huyo wa Chama cha Conservative alimpatia fedha kununulia midoli miwili kutoka duka la vifaa vya ngono mjini London mwaka 2010.

Gazeti hilo liliripoti pia kwamba Edmondson, ambaye kwa sasa anafanya kazi kwa mbunge mwingine, alisema Garnier alimweleza vibaya ikiwamo mbele ya shuhuda mmoja.

Waziri huyo wa uwekezaji anakuwa mmoja wa wanasiasa wa ngazi ya juu zaidi kutajwa na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki kwa tabia mbaya au unyanyasaji kimapenzi.

Vigogo na watu wengine mashuhuri wako matatani kufuatia mlolongo wa tuhuma za unyanyasaji na ubakaji zikiwamo zinazomkabili mfanyabiashara, ambaye kampuni yake ya utengenezaji filamu ndiyo inayotamba duniani kwa sasa, Harvey Weinstein.

Waziri wa zamani wa Chama cha Conservative, Stephen Crabb, anayefahamika kwa ulokole, alijikuta akiomba radhi baada ya gazeti kuvujisha ujumbe wa kimapenzi aliomtumia mwombaji ajira mdogo wa kike.

Hunt alisema Waziri Mkuu Theresa May atamwandikia Spika wa Bunge kushauri namna ya kubadili utamaduni huo mchafu ikiwamo rushwa ya ngono.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.