Fiesta Moshi usipime

Mtanzania - - Burudani - Na MWANDISHI WETU

BAADA ya kuwasha moto wa burudani katika Mkoa wa Tanga, wasanii mbalimbali walipanda katika jukwaa la Tigo Fiesta mjini Moshi, kuwapa burudani wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro waliofurika katika Uwanja wa Majengo juzi usiku.

Wasanii waliopanda jukwaani katika Tigo Fiesta Moshi ni pamoja na Rich Mavocal, Chege, Nandy, Maua Sama, Vanessa, Jux, Ben Pol, Aslay, Rostam, Weusi, Darassa na Lulu Diva.

Wengine ni Rose Ree, Mimi Mars, OMG, Gigy Money, Bright, Nchama, Jambo Squard na Zaiid.

Katika tamasha hilo la Tigo Fiesta, msanii Gigy Money ambaye kwa mara ya kwanza amechomoza katika tamasha hilo mkoani Tanga na Moshi, aliwapagawisha wakazi wa Moshi akiwa na wimbo wake wa ‘Nampa Papa’.

Meneja wa Tigo wanaodhamini tamasha hilo, William Mpinga, alisema kuwa hadi sasa tamasha hilo limekuwa burudani tosha kwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva na kwamba, wao wataendelea kuwajali wateja wao kwa kuwapa ofa mbalimbali lakini pia burudani.

“Tigo Fiesta 2017 kama ilivyo kauli mbiu yetu ‘Tumekusoma’, tunazidi kuwajali wateja wetu na ndio maana tunawasikliza na kuwapa kile wanachokipenda ikiwamo burudani kama hii ya kuwashuhudia wasanii wao wanaowapenda,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.