Villa Squad FC yaivuruga Cosmopolitan FC

Mtanzania - - Habari Za Michezo - Na GLORY MLAY

TIMU ya Villa Squad imeichapa Cosmopolitan mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili Taifa (SDL) , uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.

Kipindi cha kwanza cha mchezo timu zote ziliingia uwanjani kwa kasi huku kila moja ikihitaji ushindi.

Lakini mapema dakika ya 25 kipindi cha kwanza, timu ya Villa Squad ilifanikiwa kupata bao la mapema lililofungwa na Juma Chikongo, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Cosmo na kupiga shuti kali lililoingia moja kwa moja nyavuni.

Mchezo uliendelea kwa kasi huku kila mchezaji akijituma na kutumia vyema nafasi wanazozipata ambapo dakika ya 38, Villa Squad iliongeza bao la pili lililofungwa na Semi Kedira.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa timu ya Villa Squad, Abdallah Msamba, alisema licha ya kuibuka na ushindi mchezo ulikuwa mgumu kwao kwani wapinzani wao waliwakamia kupita kiasi.

Alisema wachezaji walikuwa wakipata nafasi nyingi za kufunga, lakini wameonekana kushindwa kuzitumia hali ambayo imechangia kuwa na ushindi mwembamba.

“Tunafurahi kupata ushindi, lakini bado kuna tatizo la kutofunga mabao mengi, hali hii imejitokeza baada ya kupata nafasi nane za kufunga lakini wakashindwa kuzitumia kitu ambacho bado nahitaji kukifanyia kazi,” alisema Joshua.

Msamba alisema atahakikisha anafanyia kazi makosa na mapungufu yote yaliyojitokeza ili michezo inayofuata waweze kufanya vizuri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.