Mabingwa wa soka Moro hawakamatiki

Mtanzania - - Habari Za Michezo - Na NYEMO MALECELAMOROGORO

MABINGWA wa soka Mkoa wa Morogoro, Shupavu wameendelea kuchanja mbuga katika michuano ya Ligi Daraja la Tatu kituo cha Ifakara raundi ya pili baada ya kuibamiza timu ya Mlimba City mabao 2-1.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa katika Uwanja wa Understia Ifakara, timu ya Shupavu ilitangulia kutikisa nyavu za wapinzani wao katika dakika ya 16, bao lililofungwa na Emanus Mtimalias ‘Cantona’, baada ya kupata pasi kutoka kwa Omar Halfan.

Timu ya Mlimba City ilisawazisha bao hilo katika dakika ya 55 kupitia kwa mchezaji wao, Rasta Man, jambo lililosababisha wachezaji wa timu ya Shupavu kuongeza nguvu ili kusaka ushindi.

Jitihada za timu ya Shupavu zilizaa matunda katika dakika ya 80 ambapo mchezaji, Bobrey Lukindo, alifanikiwa kuongeza bao la pili kwa kupiga mkwaju mkali.

Baada ya mchezo huo, kiongozi mwandamizi wa timu ya Shupavu FC, Athuman Kizange, aliliambia MTANZANIA kuwa timu yake inaonyesha dalili za kutetea ubingwa wa mkoa kutokana na kiwango inachokionyesha uwanjani.

“Tunaomba wadau watuunge mkono, ili tuweze kuwafanya wachezaji waweze kufanya vizuri zaidi ili tufanikishe lengo letu la kutetea ubingwa wa mkoa msimu huu,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.