Biashara Mara yainyuka Transit Camp

Mtanzania - - Habari Za Michezo - Na ESTHER GEORGE - DAR ES SALAAM

TIMU ya Biashara Mara ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Transit Camp katika mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

Katika mchezo huo kulikuwa na ushindani mkali lakini mapema dakika ya tano, Geodfrey Marcus, aliiandikia bao la kwanza timu yake ya Biashara Mara.

Bao hilo lilidumu mpaka kipindi cha kwanza cha mchezo.

Dakika ya 72 kipindi cha pili, Boniphace Selestine, alifanikiwa kuiandikia bao la pili Biashara Mara baada ya kupiga shuti kali lililopenya moja kwa moja golini.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha wa Biashara Mara, Amani Joshua, alisema licha ya kupata ushindi mchezo ulikuwa mgumu kwani wapinzani wao waliwakamia kupita kiasi lakini wakafanikiwa kupata pointi tatu ambazo anaamini zitawaweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Tumefurahi matokeo mazuri kwani mchezo ulikuwa mgumu, lakini tulipambana hivyo ninaamini mechi zinazofuata tutafanya vizuri zaidi,” alisema.

Kwa upande wa michezo mingine Dodoma FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Toto Africans uliochezwa Uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

Kutokana na matokeo hayo timu ya Dodoma FC imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa inaongoza kundi C, kwa kujikusanyia pointi 18, huku Biashara Mara ikishika nafasi ya tatu kutokana na ponti 11.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.